Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania kufanyika Novemba 19, 2024, Kufunguliwa na kufungwa na Marais

 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 14,2024 wakati wa kutambulisha Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania utakaofanyika Novemba 19, 2024.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakimsikiliza wakimsikiliza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde jijini Dar es Salaam leo Novemba 14,2024 

MKUTANO wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania kufanyika Novemba 19, 2024 jijini Dar es Salaal katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC)na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na washiriki zaidi 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwemo Mawaziri wa Madini kutoka nchi nyingine za Afrika.

Pia watahudhuria Watendaji Wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani zilizowekeza na zinazotarajia kuwekeza nchini, kama vile Kampuni ya BarrickGold, AngloGold Ashanti,  Life Zone Metals, ShantaGold, Eco Graph, Faru Graphite, HeliumOne, Lindi Jumbo, Sotta Mining, watafiti, mabalozi 31 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, mabalozi  wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi akiwemo Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Balozi Hussein Kattanga, mashirika ya kimataifa, waongezaji thamani madini, wafanyabiashara, taasisi za fedha, Vyuo Vikuu na Vya kati, Taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za madini, viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka wizara, Taasisi, Mikoa, Halmashauri na Idara za Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Novemba 14,2024 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mkutano huo amewahamasisha wadau na watanzania kutumia fursa ya uwepo wa mkutano huo kujifunza, kufuatilia na kushiriki ili kuijenga uchumi wa nchi kupitia shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya madini.

Amesema kutokana na mustakabali wa sekta ya madini nchini na duniani, mkutano huu unatarajia kuwa na jumla ya mada 8 zitakazojadiliwa kutoka kwa watoa mada wapatao 20 kutoka nje ya nchi na 35 kutoka nchini waliobobea kwenye sekta ya madini. Mada zitakazojadiliwa zitagusia maeneo mengi ikiwemo changamoto zinazokabili masuala ya uongezaji thamani madini; fursa za uwekezaji na mitaji kwenye sekta ya madini; mikakati ya uendelezaji madini mkakati kwa ajili ya kuongeza manufaa ya mnyororo wa thamani; matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo wa madini; ushiriki wa wanawake na vijana katika Sekta ya madini; kuendelea kutangaza madini adimu ya Tanzanite, na masuala mengine yakiwemo uchimbaji bora na uhifadhi wa mazingira.

Amesema kuwa kwa sasa,  kamati ya maandalizi, ipokatika hatua za kukamilisha usajili ambapo bado siku chache za kuendelea kujisajili kutokana na Mkutano huo kufanyika wiki ijayo.

 "Ili uweze kushiriki katika mkutano huo, inakupasa kujisajili kwanza kupitia tovuti ya mkutano ambayo ni conference.madini.go.tz." 

Mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Uongezaji thamani Madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii”, ambayo inalenga kuhimiza umuhimu wa uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida zaidi za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu ya taifa letu na dunia, kupandisha thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya kusafirishwa nje kwa lengo la kuchochea uanzishwaji viwanda vitakavyokuwa na manufaa nchini, kwa majirani wanaotuzunguka na duniani.

Mavunde amesema kuwa mkutano huo utakuwa na vipindi mbalimbali ikiwa pamoja na  kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi mnamo Novemba 21, 2024.  Ikitanguliwa na hafla ya usiku wa madini itakayofanyika Novemba 20, 2024 kuanzia Saa 12.30 Jioni na mgeni rasmi  atakuwa ni  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb).

Amesema mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano mingine iliyotangulia tangu kuanza kwake mwaka 2019 ambapo Serikali ilitenga zaidi ya saa sita kusikiliza kero, changamoto na maoni kutoka kwa wadau wa madini. 

"Kutokana na matokeo ya mkutano ule wa Mwaka 2019, Serikali iliona umuhimu wa  kuwa na mikutano huu yenye sura ya Kimataifa na hivi sasa, imevuka mipaka ya nchi yetu ikihusisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaohusika katika mnyororo mzima wa shughuli za madini.

"Kama mnavyofahamu kwamba, nchi yetu ya Tanzania imejaliwa utajiri wa aina mbalimbali za madini kutoka makundi karibu yote ya madini yakihusisha madini ya metali, madini mkakati, madini ya viwandani, vito vya thamani kubwa, madini yanayopatikana chini ya sakafu ya bahari kuu, ambayo yote yanaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa madini yanayohitajika duniani kote.

Kwa muktadha huo, Serikali kupitia Wizara ya Madini iliona upo umuhimu wa kuwa na jukwaa moja  linalowaleta pamoja wadau kutoka pande mbalimbali za nchi  kusikia kutoka kwetu moja kwa moja kuhusu uwepo wa rasilimali hizi  ambapo ikiwa zitatumika vizuri zinaweza kuibadili kiuchumi na kijamii Nchi yetu ya Tanzania na kuifanya moja ya Nchi zinazozalisha kwa wingi madini  duniani." Ameeeleza

Amesema mkutano huo unafanyika kila mwaka ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuendelea kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia ni jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua kwa kasi. 

Pia, unatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu Sera na mikakati mipya ya serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini, na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti, uchimbaji  na uongezaji thamani wa madini kupitia mawasilisho na maonesho kwenye mabanda yanayoenda sambamba na mkutano.

Vilevile, Mkutano huo unalenga si tu kuvutia uwekezaji, bali pia kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinawanufaisha watanzania kiuchumi na kijamii.

Licha ya hayo mkutano huo katika hafla ya usiku wa madini, kutakuwa na tukio maalum la kutambua mchango wa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini kupitia makundi mbalimbali. Hafla hiyo inalenga kutambua mchango wa wadau hawa katika maendeleo na ukuaji wa sekta, huku ikihamasisha wadau wengine kuongeza juhudi, kuziona fursa zilizopo na kuchangia katika mafanikio ya sekta ya madini nchini. Pia, usiku wa madini huambatana na onesho la bidhaa za madini ya vito. 

Post a Comment

Previous Post Next Post