WAZIRI MHAGAMA: TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA AFYA

 

Na WAF – Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Novemba 13, 2024 amekutana na Mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (World Health Organization- WHO) Dkt. Charles Sagoe-Moses kwa mara ya kwanza kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Afya.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam Waziri Mhagama ameishukuru WHO kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na changamoto za magonjwa ikiwemo magonjwa ya milipuko. 

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nachukua fursa hii kuwashukuru Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa msaada na ahadi zenu mlizozitoa katika kusaidia na kuboresha huduma za afya nchini,” amesema Waziri Mhagama

Shirika la Afya Duniani pamoja na Tanzania zimekuwa zikishirikiana kwa miongo kadhaa katika kuboresha Sekta ya afya katika maeneo ya ushirikiano wa kiufundi, mijadala ya kisera, ushauri pamoja na kubadilishana maarifa kwa wataalamu wa afya. 

Pamoja na mambo mengine Waziri Mhagama ameomba ushirikiano katika suala la Bima ya Afya kwakuwa Sekta ya Afya imefikia hatua muhimu ya kuanza kwa utekelezwaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni njia ya kusaidiana ili watu wa hali ya kipato cha chini wapate matibabu bila kikwazo cha fedha.

“Tunashukuru kwa ushirikiano wa pamoja na Shirika la Afya Duniani lakini pia tunaomba ofisi yako iendelee kuunga mkono na kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikiwa,” amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama amelihakikishia Shirika hilo kuwa Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kutimiza azma ya kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Charles Sagoe-Moses wakati akijitambulisha kwa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania hasa katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika na kuwalinda na magonjwa hasa ya mlipuko kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya kuwezesha utolewaji wa elimu.      

Post a Comment

Previous Post Next Post