Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZALISHAJI wa maziwa na bidhaa zake nchini wameshauriwa kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) hatua ambayo itawawezesha kuaminika na kuhimili ushindani kwenye soko.
Wito huo ulitolewa na Afisa Udhibiti ubora TBS,Bw.Donald Mkonyi kwenye Maadhimisho ya 27 ya Wiki ya Maziwa kitaifa yaliyoanza Mei 28 na kumalizika Leo Juni 1, mwaka huu kwenye viwanja Furahisha wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Mkonyi alisema TBS imeshiriki maadhimisho hayo kwa lengo la kusogeza huduma kwa wazalishaji maziwa na bidhaa zake kwa kuwapatia elimu ili waweze kufika TBS kuthibitisha bidhaa zao ziweze kushindana ndani na nje ya nchi.
Alifafanua kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeingia makubaliano, ambapo bidhaa zikishathibitishwa ubora na mashirika ya viwango ya nchi hizo, zinapovuka mipaka kwenda nchi nyingine hazitakiwi kupimwa tena, hivyo hiyo ni fursa muhimu kwa wazalishaji wa maziwa na bidhaa zake kuweza kufikia masoko ndani na nje ya nchi pasipo kukumbana na vikwazo vya kibiashara.
Mkonyi, alisema huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa kwa wajasirimali inatolewa bure na TBS, kwani kila mwaka Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inatenga fedha kwa ajili hiyo.
Aliongeza kwamba TBS inatambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi, ndiyo maana shirika hilo lina utaratibu endelevu wa kutoa elimu kwa wajasiriamali, kwa kuzingatia kwamba utoaji elimu ya viwango ni moja ya majukumu ya shirika hilo.
"Tumekuwa tukitoa elimu hiyo kwa wazalishaji wote ili waweze kupata alama ya ubora," alisema Mtemvu. Alisema kupitia maadhimisho hayo walitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na majukumu ya shirika.
Awali akifungua maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwahamasisha wananchi kuongeza kasi ya unywaji maziwa yaliyothibitishwa ubora, kwani yanakuwa salama kwa afya ya watumiaji.