KAMATI YA BUNGE PIC YAIPA KONGOLE REA KWA KASI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC), Augustino Vulu, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembea mradi huo wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2) katika vijiji vya Irisya, Masutianga na Munyu vilivyopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida, Aprili Mosi, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC) imewapongeza  Wakala wa Nishati Vijijini (REA)  kwa mradi wa usambaji wa a umeme katika vijiji vitatu vilivyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida..

Vijiji vilivyonufaika katika mradi huo ni Munyu, Irisya na Masutianga vyote vikiwa Kata ya Irisya wilayani humo.

Wajumbe hao wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa PIC, Augustino Vulu wametoa pongezi hizo Aprili 1, 2023 baada kutembelea mradi huo wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2) ambao umeonesha kuleta tija kwa wananchi.

Vulu alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh. bilioni 50 kwa ajili ya kukamilisha miradi minne inayotekelezwa mkoani humo miradi ambayo ikikamilika itakuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi.

“Leo tupo hapa Shule ya Sekondari ya Irisya ambapo tumeshuhudia jinsi wanafunzi na wananchi wanaoishi katika kijiji hicho jinsi walivyoanza kunufaika baada ya kupata umeme ambao umewekwa kwenye madarasa na wanafunzi kuanza kujisomea hadi usiku.” alisema Vulu.

Vulu alisema wanatarajia kuona ufaulu ukiongezeka kwa wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi kwani hivi sasa watakuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo baada ya kupata umeme.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene alisema mradi huo umeanza kuleta faida katika Shule ya Sekondari ya Irisya na vijiji hivyo vitatu vinavyopakana na shule hiyo na lengo likiwa nikuona umeme huo unawasaidia, kiuchumi, maendeleo kwa maana ya elimu na mambo mengine.

“Kuletwa umeme katika vijiji hivi sisi kwetu ni furaha na tunajua sasa tumetimiza wajibu wetu kuhakikisha kuwa yale malengo tuliojiwekea yanatimia” alisema Ndeme.

Ndeme aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo ya kuwekewa umeme kwa kujiunganisha kwenye maeneo yao ya makazi na biashara na wabuni biashara ambazo zinatumia umeme kwa ajili ya kujinufaisha kwa kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja, vijiji, wilaya nzima na mkoa kwa ujumla.

Aidha Ndeme amewaomba wananchi wa maeneo hayo yaliyopata umeme kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao wanayolima kwa kuyachakata na kuyaongezea thamani na kujikuta wakikua kiuchumi. 

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Singida kwa Kamati, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala hiyo imetoa jumla ya shilingi bilioni 73.1 na Dola za Marekani 988,707.60 ili kuhakikisha miradi minne inayotekelezwa mkoani humo inakamilika na wananchi wanapatiwa huduma ya nishati hiyo ili kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Aidha, ameeleza zaidi kuwa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Wilaya za Ikungi na Singida unatekelezwa na Mkandarasi M/s Central Electricals International Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 26.3 na katika Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, unatekelezwa na M/s CRJE – CTCE Consortium kwa gharama ya shilingi bilioni 31.6 

Amesema kuwa, maendeleo ya Mradi kwa wastani yamefikia asilimia 70.21 ambapo kwa Wilaya za Ikungi na Singida, Mkandarasi amefikia asilimia 77.54 na Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, Mkandarasi amefikia asilimia 62.87. 

Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo vijiji 287 vimekwishapatiwa umeme kupitia miradi ya umeme vijijini iliyotekelezwa awali. Vijiji 169 vilivyobaki vinaendelea.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na REA katika kazi hiyo ya kutoa huduma kwa wananchi na ndio maana ilipo REA na TANESCO ipo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene, akizungumzia manufaa ya mradi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza kwenye ziara hiyo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga akizungumza kwenye ziara hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye ziara hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakiwa kwenye ziara hiyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post