Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tuzo ya kutambua mchango wake wa kuanzishwa kwa Taasisi hiyo iliyotolewa wakati wa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza, Beach jijini Dar es Salaam mwezi wa pili mwaka huu.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge kuhusu mchakato wa kuanzishwa kwa Taasisi hiyo jinsi ulivyofanyika wakati alipokutana na uongozi wa JKCI ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimweleza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete jinsi huduma za matibabu ya moyo zinavyotolewa katika Taasisi hiyo wakati walipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umuhimu wa kushirikiana na mashirika ya kimataifa ambayo yanaujuzi mkubwa wa kutibu magonjwa ya moyo zaidi yao wakati alipokutana na uongozi wa Taasisi hiyo ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge.
*******************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma bora za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi.
Pongezi hizo amezitoa leo alipokutana na Uongozi wa Taasisi hiyo ofisini kwake jijni Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Kikwete alisema kabla haijaanzishwa Taasisi hiyo Serikali ilikuwa inatumia fedha nyingi kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi hivyo kuamua kujenga JKCI ili wananchi wapate huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini.
“Mchakato wa kujenga Taasisi ya Moyo ulianza taratibu hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kujenga jengo la kutolea huduma pamoja na kununua vifaa vya kisasa vya kutolea huduma hiyo.
“Leo hii ninafurahi kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinapatikana hapa nchini, wagonjwa wote walio na fedha na wasio na fedha za kulipia huduma wanatibiwa kwa wakati”, alisema Dkt. Kikwete.
Aidha Mhe. Dkt. Kikwete aliitaka Taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa ambayo yamepiga hatua zaidi katika matibabu ya moyo, kwa kufanya hivyo wataongeza ujuzi zaidi kwani ukishirikiana na wanaojua kukuzidi utafanya vizuri zaidi.
“Unaweza kuwa na jengo zuri pamoja na vifaa vya kisasa ukashindwa
kutoa huduma kwani huna utaalamu wa kutosha lakini kama utashirikiana na watu wenye utaalamu zaidi utaweza kujifunza kutoka kwao na kutoa huduma bora”.
“Katika muda mfupi tangu ianzishwe Taasisi hii imefanya vizuri na kuaminika ndani na nje ya nchi endeleeni kushirikiana na wenzenu waliowazidi ili mpate ujuzi wa kutosha na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, moja ya faida ya kushirikiana na mashirika haya wanakuja na ujuzi pamoja na vifaa vya kisasa vya kutolea huduma za matibabu”, alisisitiza Dkt. Kikwete.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge
alimshukuru Mhe. Dkt. Kikwete kwa kukutana nao na kumuahidi wafanyakazi wa Taasisi hiyo wataendelea kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.
Dkt. Kisenge pia alimkabidhi Mhe. Dkt. Kikwete tuzo ya kutambua mchango wake wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyotolewa wakati wa mkutano wa kwanza wa shambulio la moyo uliofanyika katika Hoteli ya Ledger Plaza, Beach jijini Dar es Salaam mwezi wa pili mwaka huu.