TAWA YATEKELEZA MAAGIZO YA RAIS DKT. SAMIA YA KUDHIBITI WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU KWA KUWAVALISHA TEMBO VISUKUMA MAWIMBI.

 

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) imetekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa Disemba 1, 2022 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika Mkoani Lindi.

Maagizo hayo ni kuhakikisha kuwa madhara yaletwayo na wanyama wakali na waharibifu yanadhibitiwa ipasavyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo leo Disemba 3, 2022, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amesema, zoezi hili la kuwavalisha tembo visukuma mawimbi litasaidia kuondoa madhara yaletwayo na wanyama hao kwa sababu , vifaa hivyo vinafuatilia mienendo ya tembo na vitawaongoza askari katika zoezi la kuwarudisha hifadhini kabla hawajafika katika makazi ya wananchi.

Vilevile, Naibu katibu Mkuu amewasihi wananchi kuwa watulivu kwa kipindi hiki ambacho zoezi hili la uvishaji wa kola na kuwaswaga makundi ya tembo kurudi hifadhini linaendelea.

Naye, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TAWA, amesema sambamba na zoezi hilo TAWA imetoa mafunzo ya kijeshi kwa vijana wanaoishi pembezoni mwa hifadhi yani Village Game Scouts (VGS) watakaotumika kama Askari wa Akiba katika kukabiliana na changamoto ya wanyama hawa hususan katika vijiji ambavyo matukio ya kuvamiwa na tembo yamekuwa yakijirudia.

Kadhalika, TAWA imenunua pikipiki ambazo zimefungwa vifaa maalumu vya kutoa matangazo kwa wananchi. Pikipiki hizo zitatumika katika maeneo ambayo magari ya doria hayawezi kuyafikia.

Naibu Kamishna Kabange aliongeza kuwa TAWA imekamilisha ujenzi wa nyumba za askari ambazo zimejengwa katika vijiji vya Nditi na Ngumbu vilivyopo katika wilaya za Nachingwea na Liwale. Vijiji hivi vimekuwa vikipata changamoto kubwa ya wanyama wakali na waharibifu.

TAWA inashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzaniahi (TAWIRI) kwenye zoezi hilo la ufungaji wa visukuma mawimbi na la kurudisha makundi ya tembo kutoka vijiji vilivyopo Mkoani Lindi na kuwarudisha hifadhini.

   

Post a Comment

Previous Post Next Post