WAZIRI MBARAWA AMTAKA MKANDARSI BARABARA YA RUANGWA-NANGANGA KM 53.2 KUONGEZA KASI


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Lindi Mhandisi Ezra Magogo kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mzani katika eneo la Mnazi Mmoja Mkoani Lindi, wakati Waziri huyo alipokagua mradi huo.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mzani wa Mnazi Mmoja Mkoani Lindi. Mzani huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Mkuu wa Wilaya wa Ruangwa, Hassan Ngoma kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga yeye urefu wa Kilomita 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wakati Waziri huyo alipokagua mradi huo Wilayani humo Mkoani Lindi.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa Kilomita 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha Lami, Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wilaya ya Ruangwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Lindi wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa Kilomita 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

PICHA NA WUU

…………………………….

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi anayejenga barabara ya Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilomita 53.2 kuongeza kasi ili ifikapo April mwakani barabara hiyo iwe imekamilika.

Barabara hiyo inayojengwa na Mkandarasi China Railway 15 bureau Group Coorporation ni sehemu ya barabara ya Nachingwea-Ruangwa-Nanganga yenye urefu wa kilomita 106 ambayo ikikamilika itafungua wilaya za Masasi, Nachingwea na Ruangwa kiuchumi.

Akizungumza mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo Prof. Mbarawa amesema kukamilika mapema kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kutaiwezesha Serikali kuendelea na ujenzi wa barabara za lami katika ukanda huo na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Amemtaka Mkandarasi China Railway 15 bureau Group Coorporation anayejengwa barabara hiyo kufanya kazi usiku na mchana na kuitaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Lindi, kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa ubora uliokusudiwa. 

“Eneo hili ni muhimu sana kwa shughuli za madini ya graphite na kilimo, hivyo barabara hii itakapokamilika itawaunganisha vizuri wananchi wa mkoa wa Lindi na wilaya zake” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Prof Mbarawa amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha mkoa wa lindi unafunguka katika njia zote ili fursa zote mkoani humo ziweze kutumika kikamilifu kuwanufaisha wananchi.

Aidha, katika hatua nyingine amekagua ujenzi wa mzani mpya eneo la Mnazi mmoja kwenye barabara ya Mingoyo hadi Masasi na kuitaka TANROADS kuhakikisha mizani hiyo inakamilika mwishoni mwa mwezi huu ili kupunguza msongamano wa magari yanayotoka Songea kwenda Mtwara na Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Lindi Mhandisi Ezra Magogo amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa mradi wa mzani utakamilika mwishoni mwa mwezi huu ili kuondoa msongamano uliokuwepo awali katika eneo la mnazi mmoja na kuvutia zaidi wawekezaji zaidi mkoani humo. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa na kumueleza kuhusu kuridhishwa na ujenzi wa Barabara hiyo inayounganisha wilaya  hiyo na barabra kuu ya Mingoyo-Masasi na hivyo kukamilika kwake kutachochea uchumi wa Wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Masasi.

Barabara ya Nachingwea-Ruangwa- Nanganga yenye urefu wa KM 106 imegawanywa katika sehemu mbili ikiwemo Nachingwea hadi Ruangwa KM 50 na Ruangwa hadi Nanganga KM 53.2 ambapo katika sehemu ya pili zaidi ya shilingi bilioni 50 zinatarajiwa  kutumika.

Profesa Makame Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu (3) katika mikoani ya Mtwara na Lindi kukagua miradi ya sekta za ujenzi na uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post