NA MWANDISHI WETU,
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema kwa sasa wapo katika mchakato wa kutoa elimu ya kodi kwa viongozi wa dini wa madhehebu yote hapa nchini.
Kiongozi huyo wa TRA, ametanabaisha hayo leo, Januari 2, 2025 mbele ya Mufti ambaye pia ni Sheikh Mkuu Tanzania, Dkt Abubakar Zuber, alipotembelea Ofisi za Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Hatua hii ya kutoa elimu kwa viongozi wa dini itasaidia kuhamasisha elimu hiyo kwa waumini wao jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo kwa taifa kwa kuwa jamii kubwa itakuwa inafahamu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari”, amesema.
Pia ameongeza kuwa kulipa kodi ni ibada na taasisi za kidini zina fursa kubwa ya kuhamasisha waumini wao kulipa kodi kwa hiari kwa lengo la kuleta maendeleo kwa taifa.
Mwenda ameongeza kwamba licha ya Bakwata kuwa taasisi ya kidini, pia kwa njia moja au nyingine inajihusisha na shughuli mbalimbali ambazo zinawajibisha ulipaji kodi na huu ndio wakati wa kuhamasisha waumini wao kulipa kodi kwa hiari kupitia majukwaa ya kidini.
Naye Sheik Mkuu, Dkt,, Dkt Abubakar Zuber, ameipongeza na kuishukuru TRA kwa kufika ofisini kwake na kufafanua kwamba ni muhimu kwa viongozi wa dini kupata elimu hiyo ambayo nao wataifikisha kwa waumini wao itakayosaidia kutawanya elimu ya mlipa kodi kwa kundi kubwa kwa wakati mmoja.
Pia Mufti Dkt, Zuber alichukua fursa ya kukutana na Kamishna Mwenda kujadiliana namna ya kutumia njia bora za kutanua wigo wa ulipaji kodi.