RUWASA YAENDELEA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI,YAKAMILISHA UJENZI WA MRADI WA MAJI KIJIJI CHA NEGHABIHI,IRINGA

 Na Muhidin Amri,Iringa


SERIKALI kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa kushirikiana na shirika la AMREF/USAID ,imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Neghabihi Halmashauri ya wilaya Iringa mkoani Iringa, na kumaliza kero kwa wananchi kuendelea kutumia maji ya mto Ruhaha ambayo siyo safi na salama.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,Meneja wa Ruwasa wilaya ya Iringa Masoud Samila alisema,kijiji hicho hakijawahi kuwa na maji ya bomba tangu Uhuru, badala wananchi walilazimika kutumia maji ya mto mdogo wa Ruhaha na vyanzo vingine visivyo rasmi.

Samila alisema kuwa,mradi wa maji Nyamlenge(Neghabihi) ni wa teknolojia ya msukumo kwa kutumia pampu ya umeme na chanzo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 15,230 kwa saa.

Alisema,lengo la mradi ni kuwapatia wananchi wa vijiji hicho na vijiji jirani huduma ya maji safi na usalama ndani ya umbali usiozidi mita 400 na utakapokamilika utawanufaisha zaidi ya wakazi 1,675 wa kijiji cha Neghabihi.

Alisema,kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa tenki la lita 150,000 kwenye mnara wa mita 9,kuchimba mtaro,kulaza na kufikia bomba urefu wa km 10.24,kujenga vituo 11 vya kuchotea maji na kujenga nyumba ya mashine(Pump House).

Alitaja kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa tenki,kuchimba na kulaza mabomba umbali wa km 9.95,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji na nyumba ya mashine ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 100 na wananchi wameanza kupata huduma ya maji.

Alisema,mradi unatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya M/S GNMS Controctars Co. Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 664,125,422.43 kati ya hizo, serikali kuu kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano ya Uvico-19 imetoa Sh.milioni 511,370,172.73 na AMREF/USAID imetoa Sh.milioni 132,755,250.00.

Alitaja vijiji vingine vitakavyonufaika na mradi huo ni Magulilwa chenye wakazi 5,216 kijiji cha Mlanda chenye wakazi 2,672 na Nyabula chenye wakazi 4,625 ambavyo vinatarajiwa kufikishiwa maji ya bomba na Ruwasa iko kwenye hatua za mwisho kukamilishaji maandalizi ya mkataba ili kuwezesha utekeleza wa mradi katika vijiji hivyo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Haule Msigala alisema, wameupokea vizuri mradi kutokana na adha ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji chao.

Aidha,amehaidi wananchi na serikali ya kijiji hicho itahakikisha inatunza mradi na miundombinu yake ili uweze kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,ametoa wito kwa viongozi wa serikali ya kijiji hicho kujipanga kuona namna gani wanavyoweza kulinda miundombinu ya mradi na chanzo cha maji kitakachotumika kwa kuzalisha maji.

Alisema fedha zilizotumika kujenga mradi huo ni nyingi, kwa hiyo wananchi ni lazima wautunze
na wauone ni wa kwao ili uweze kudumu kwa mradi mrefu, badala ya kuendelea kutumia maji ya mto Ruhaha.

Amewapongeza wafanyakazi wa Ruwasa wilaya na mkoa wa Iringa,kwa kusimamia vizuri na kukamilisha mradi huo na kuwataka wananchi wa kijjiji hicho kuanza kuchangia huduma ya maji nakutumia maji hayo kwa shughuli zao za maendeleo.

Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo katikati,akikagua kisima cha maji kwenye mradi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Neghabihi wilaya ya Iringa unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na AMREF/USAID kwa gharama ya Sh.milioni  664,125,422.43 wa pili kulia Meneja wa Ruwasa mkoa wa Iringa Joyce Bahati na wa pili kushoto meneja wa Ruwasa wilaya ya Iringa Masoud Samila.


Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo akifungua koki kwenye mradi wa maji kijiji cha Neghabihi Halmashauri ya wilaya Iringa  mkoani Iringa alipotembelea mradi huo ili kuona utekelezaji wake,kushoto meneja wa Ruwasa mkoani Iringa Joyce Bahati.
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Iringa Mhandisi Joyce Bahati kulia,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo baada ya kutembelea mradi wa maji katika kijiji chaNeghabihi wilayani Iringa unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na AMREF/USAID kwa gharama ya Sh.milioni  664,125,422.43 ,wa kwanza kushoto Mkurugenzi wa Ufundi wa Ruwasa Mhandisi Ndele Mengo na wa pili kushoto Mkurugenzi wa Usambazaji maji safi na usafi wa mazingira Wizara ya maji  CPA Joyce Msiru.

Post a Comment

Previous Post Next Post