Ngusa: Wananchi Wa Lindi Tumieni Vizuri Ujio Wa Madaktari Bingwa Wa Moyo Kuchunguza Afya Zenu

 Na: Mwandishi Maalum

 Wananchi wa Mkoa wa Lindi wameombwa kutumia vizuri ujio wa madaktari mabingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya hayo kwani mkoa wa Lindi upo mbali na hospitali kubwa za kibingwa tofauti na ambavyo mikoa mingine ilivyo.


Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ngusa Samike alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine (SRRH) kufungua kambi maalum ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayoende katika Hospitali hiyo.

Ngusa alisesma wananchi wa Lindi waliokuwa na hamu ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo sasa wamepata nafasi ambayo imewasaidia kupunguza gharama za kufuata huduma hizo zinazopatikana nje ya Mkoa wa Lindi.

“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ubunifu wa hali ya juu kuendesha zoezi la kuwafikia wananchi kupata huduma za matibabu ya moyo jambo ambalo linaleta thamani katika maisha ya binadamu”, alisema Ngusa

Ngusa alisema uelewa wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa Lindi upo chini hivyo mara nyingi wanapojisikia kusumbuliwa na matatizo tofauti tofauti huona ni jambo la kawaida lakini kwa ujio wa wataalam kutoka JKCI kutawasaidia wananchi hao kutambua magonjwa mbalimbali na kuona umuhimu wa kuchunguza afya zao mara kwa mara.

Aidha Ngusa alisema Mkoa wa lindi ni mkoa wa tatu kwa ukubwa ukiacha mkoa wa Tabora na Mkoa wa Morogoro hivyo kuwaomba wataalam kutoka JKCI wakati mwingine wanavyoandaa matibabu kama hayo waufikirie Mkoa huo ulivyo na eneo kubwa na kupeleka huduma eneo ambalo litawakutanisha wananchi wengi zaidi ili wananchi hao waweze kufaidika.

“Kijografia jinsi Mkoa wetu ulivo ni ngumu sana kwa hapa lindi mjini kuwapata wananchi wa Liwale, Ruangwa na Nachingwea ambapo idadi ya watu ni kubwa zaidi katika Mkoa wetu hivyo tunawaomba kipindi kingine mtakaporudi tena mjipange ili tuweze kutoa huduma kuendana na jografia ya eneo letu na wananchi wengi zaidi wafaidike na huduma hizi”, alisema Ngusa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya alisema JKCI imeweka mpango wa kuzunguka mikoa mbalimbali ya Tanzania kusogeza huduma kwa wananchi ili waweze kujitambua na kuchukua tahadhari mapema.

“Katika kambi za matibabu tunazozifanya tumekua na malengo manne makubwa ambayo ni kuwafikishia huduma za matibabu ya moyo wananchi walipo, kutoa elimu ya magonjwa hayo, kushirikishana uzoefu na wataalam wenzetu wa afya pamoja na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo kulingana na maeneo na mikoa tunayotembelea”,

“Tunawaomba wananchi kubadilisha mfumo wao wa maisha ili kuepukana na magonjwa haya yasiyoambukiza hasa magonjwa ya shinikizo la juu la damu tatizo ambalo limeonekana kuwa kubwa kwani shinikizo la juu la damu hupelekea moyo kutanuka, kupata kiharusi na kuleta shida nyingine nyingi katika mwili wa binadamu”, alisema Mallya

Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo maalum ya matibabu ya moyo Amina Ngumbe amewaomba wataalam kutoka JKCI kufika katika Mkoa huo mara kwa mara kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwani wananchi wengi wanahitaji huduma hizo.

“Mimi mwenyewe nilikua nampango wa kwenda Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya moyo lakini nilivyosikia wanakuja Lindi nikafarijika sana, Nawaomba waweke ratiba za kutuhudumia mara kwa mara ili tusihangaike kuwafuata wakati tunaumwa”, alisema Amina

Amina alisema kwa watalam hao kufika mkoani Lindi kunatoa motisha kwa wananchi kuchunguza afya zao kwa wakati kwani mara nyingi wananchi wengi huwa hawachunguzi afya zao hadi wanapozidiwa ndio hutafuta huduma za matibabu.

Mbali na wataalam wa JKCI waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine kutoa huduma za matibabu wataalam hao pia wanatoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo pamoja na kubadilishana uzoefu na wataalam wa afya wa Hospitali ya Sokoine kujenga uzoefu wa ndani wa kutoa huduma hizo kwa wananchi.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Josephat Katoto akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi wa mkoa wa Lindi aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine (SRRH) wakati wa kambi maalum ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SRRH.

Picha na: JKCI

: Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Khairoon Mohamed akimfanyia uchunguzi mama ambaye amepata kiharusi wakati wa kambi maalum ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine (SRRH).

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Letara akimwelezea Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ngusa Samike huduma zinazotolewa kwa watoto wenye magonjwa ya moyo alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine (SRRH) kwa ajili ya kufungua kambi maalum ya siku tatu ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SRRH. Wanne kutoka kushoto ni Mganga Mfawidhi wa SRRH Dkt. Mohamed Muhaji

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ally Athuman akimpima shinikizo la damu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ngusa Samike alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine (SRRH) kwa ajili ya kufungua kambi maalum ya siku tatu ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa SRRH

Post a Comment

Previous Post Next Post