MAKAMU WA RAIS KUMWAKILISHA RAIS SAMIA TAMASHA LA 41 LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTAMADUNI BAGAMOYO

 MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), linalotarajiwa kuanza Novemba 10, mwaka huu mjini humo.Dk. Mpango atakuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo msimu huu, kwa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Hassan Abbasi, alisema walitarajia Rais Samia awe mgeni rasmi lakini atawakilishwa na Makamu wa Rais, Dk Mpango.

Dk.Abbasi alisema ni heshima kubwa kuandaa tamasha hilo ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka na maandalizi yanakwenda vizuri.Alisema wa Dk. Mpango atakuwa mgeni rasmi na kwamba tamasha litafanyika kwa ukubwa wake ili kuendelea kulipa heshima kwani litashirikisha vikundi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Uzinduzi utafanyika Novemba 10, mwaka huu na jioni yake tamasha litaanza rasmi ambapo litashirikisha vikundi vya ndani na nje ya nchi.“Mgeni rasmi tunatarajia atakuwa Makamu wa Rais Dk. Mpango ambaye atamwakilisha Rais Samia, kutakuwa na burudani za kila aina na nchi mbalimbali zimeshathibitisha ushiriki wao.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutupa heshima hii kama wizara na kamati itakuwa huru kwa wadau wote wakiwemo nchi marafiki na mabalozi wa nchi mbalimbali,” alisema Dk. Abbasi.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallah alisema anawakaribisha wadau mbalimbali wa burudani katika tamasha hilo.Alisema tamasha la mwaka huu linatarajiwa kuwa tofauti zaidi kwani kutakuwa na tukio la Royal Tour ambapo wadau wa sanaa watatembelea vivutio mbalimbali vya Bagamoyo.

Alisema pia yeye na viongozi mbalimbali watakaohudhuria watatoa burudani ya aina yake kutokana na taswira ya tamasha la TaSUBa.“Tunawakaribisha wadau mbalimbali kujitokeza kwa ajili ya kupata burudani katika tamasha la mwaka huu, maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na tutahakikisha kila mmoja atakayehudhuria ataondoka akiwa ameridhika.“Mimi na viongozi wenzangu ambao tutakuwepo, tunatarajia kutoa burudani ya aina yake katika tamasha la mwaka huu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Herbert Makoye alisema jumla ya vikundi 27 vya Tanzania vimethibitsha kushiriki huku nane vikitoka nje ya nchi.

Alisema kuwa wameshapata ufadhili kutoka katika maeneo mbalimbali huku wakiendelea kuzungumza na wadau wa sanaa ili kuwaunga mkono.Aliongeza tamasha hilo litakuwa la aina yake kwani lina hadhi ya kimataifa na litashirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali.

“Tunaendelea na maandalizi ya tamasha la mwimu huu ambapo litahusisha vikundi 27 kutoka Tanzania na vingine nane kutoka nje ya nchi.“Kila kitu kinakwenda vizuri kwani tumeshapata ufadhili kutoka kwa watu mbalimbali na tunaendelea kuzungumza na wadau ili watuunge mkono,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Siku ya Tamasha la 41 la Utamaduni Bagamoyo (Bagamoyo Festival) ambalo linatarajia kufanyika Novemba 10 kwenye Viwanja vya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dkt. Herbert Makoye na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainabu Abdallah Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Siku ya Tamasha la 41 la Utamaduni Bagamoyo (Bagamoyo Festival) ambalo linatarajia kufanyika Novemba 10 kwenye Viwanja vya TaSUBa Bagamoyo mkoani Pwani

Post a Comment

Previous Post Next Post