Na John Mapepele, Leicester
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ametembelea miundombinu ya michezo nchini Uingereza na kufanya mazungumzo na wamiliki wake lengo likiwa ni kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
Katika ziara hiyo aliyoifanya Julai 30, 2022, Mhe. Mchengerwa ametembelea kiwanja cha King Power na St Mary’s kinachomilikiwa na klabu ya Southampton na kujionea miundombinu mbalimbali ya michezo na kujifunza namna bora ya kuiendeleza na usimamizi wa miundombinu hiyo.
“Tumejifunza mambo mambo mengi makubwa ambayo sisi pia tunaweza kuyaiga na kuyaboresha kutoka kwa wenzetu hawa ambao wamepiga hatua kubwa kwenye anga ya michezo na sisi tukapiga hatua ya haraka” amefafanua Mhe. Mchengerwa
Akiwa kwenye ziara hiyo Mhe. Mchengerwa alipata fursa ya kushuhudia fainali za kombe la ngao ya jamii mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa King Power katika mji wa Leicester baina ya timu ya Liverpool na Manchester City ambapo Liverpool imeibuka mshindi wa kombe hilo kwa kuibamiza Manchester City Magoli matatu kwa nunge.
Mara baada ya kutembelea miundombinu hiyo, Mhe. Mchengerwa ameelezea kuwa Tanzania inakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye michezo kwa kuimarisha miundombinu yake ili kuwa na maeneo ambayo yatazalisha wachezaji wengi ambao watakuwa kwenye kiwango cha kimataifa.Mhe. Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuona kuwa michezo inakua kwa kasi kubwa na kutoa ajira kwa watanzania wengi lengo likiwa ni kuchangia kwenye uchumi wa taifa kwa ujumla.
Aidha, Mhe Mchengerwa ametumia nafasi hiyo kukutana na wachezaji nguli wa Tanzania wanaoishi nchini Uingereza na kubadilishana mawazo viongozi mbalimbali wa michezo na kufanya majadiliano ya kuimarisha sekta ya michezo nchini.Miongoni mwa wananmichezo hao ni Abdallah Shamuni na Hussein Mwakuluzo.
Katika ziara hiyo Mhe. Mchengerwa aliambatana na Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na maendeleo, Musa Sima na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu.
Akiwa huku amempongeza mwanariadha wa Tanzania kwenye timu ya wanamichezo wanaoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola Alphonse Felix SIMBU kwa kunyakua medali ya fedha na kusisitiza kuwa medali aliyoipata ni heshima kubwa kwa taifa la Tanzania.
Awali kabla ya mashindano Mhe. Mchengerwa alitembelea kambi ya kikosi cha wanamichezo wa Tanzania na kuwapa hamasa kubwa ya kuwataka watangulize uzalendo wa nchi yao kwa kucheza kufa na kupona ili kuitangaza Tanzania kupitia michezo.