Mh. MCHENGERWA ATOA NENO MECHI YA SIMBA NA YANGA


Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa  leo Mei 1, 2022 amezipongeza timu za Simba na  Yanga kwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa ligi kuu ya NBC wa jana Uwanja wa Benjamin Mkapa huku akiwataka wachezaji kuwa na nidhamu wakiwa uwanjani ili timu ziweze kufika mbali kwenye mashindano ya kimataifa.

Amesema kiwango kilichoonyeshwa na timu zote kimetia matumaini kuwa soka la Tanzania limeendelea kukua kutokana na timu zote mbili kuonyesha ushindani mkubwa kimchezo.

Mhe. Mchengerwa amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kuboresha miundombinu ya michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri.

Mhe, Mchengerwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye mechi hiyo amefafanua kuwa kwa sasa Serikali imeendelea kugharimia kuziweka kambini timu zote za taifa zinazoendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.

"Nisisitize tu kuwa Serikali kwa sasa imeshatenga fedha nyingi kuziwezesha timu zote za michezo mbalimbali ili zifanye vizuri zaidi na kupeperusha bendera ya taifa letu kwenye mashindano ya kimataifa". Ameongeza Mhe, Mchengerwa 

Aidha, amesema katika kipindi hiki Serikali inakwenda kusaka vipaji vya wanamichezo kupitia program ya ligi ya mama Samia ya Mtaa kwa mtaa.

Mchezo wa jana ulihudhuriwa na  viongozi mbalimbali wa Serikali na michezo na mashabiki ambao walifurika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo timu zote hazikufungana.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mechi hiyo ni pamoja na Waziri wa TAMISEMI. Mhe, Innocent Bashungwa,  Mawaziri kutoka Tanzania Visiwani, Naibu Spika na Mbunge wa Ilala,  Mhe. Musa Zungu, Mkurugenzi wa Michezo Yusufu Singo na wadau mbalimbali.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post