Na.Mwandishi Wetu,
TUME ya Ushindani (FCC) imetunukiwa tuzo maalum ya kutambua mchango wake katika maendeleo ya Sekta ya Manunuzi na Ugavi nchini.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, na kupokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha FCC, Bi. Roberta Feruzi.
Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ilifanyika katika Kongamano la 16 la Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha lililoandaliwa na Bodi ya Wataalamu na Mafundi wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).
FCC imeshiriki kongamano hilo kama mdau muhimu wa sekta ya manunuzi na ugavi, ambapo iliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki katika masuala ya manunuzi na ugavi, hususan katika kulinda mnyororo wa thamani.
Kupitia kongamano hilo, Tume pia ilitoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu majukumu na kazi zake, ikisisitiza nafasi yake katika kuhakikisha mazingira ya ushindani yanayochochea uwazi, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya manunuzi na ugavi nchini.


