Waziri Wa Maliasili Na Utalii Atembelea Eneo La Hifadhi Ya Ngorongoro Na Loliondo Kukagua Shughuli Za Uhifadhi Na Utalii .

 Mwandishi wetu, NCAA.


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 6 aprili, 2022 amefanya ziara katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Loliondo Mkoani Arusha kwa lengo la kukagua shughuli za Uhifadhi, Utalii na miradi mbalimbali ya ukarabati wa miundombinu ya barabara.

Katika ziara hiyo Mhe. Chana ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa juhudi za uhifadhi wa mazingira, ulinzi wa wanyamapori, ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za utalii kwa wageni wanaotembelea eneo hilo.

“Nimetembelea eneo la Hifadhi ya Ngorogoro na Loliondo ili kujionea kazi kubwa inayofanywa ya kuhifadhi, kulinda Wanyamapori, kuendeleza shughuli za utalii na ukarabati wa miundombinu ambayo serikali imekuwa ikitoa fedha, nashukuru uongozi wa NCAA unasimamia vizuri na nimeona kazi kubwa inaendelea kufanyika” alifafanua Dkt. Chana.

Mhe. Waziri ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Hifadhi ya Ngorongoro inalindwa kwa njia zote kama moja ya maeneo muhimu ya urithi wa dunia na chanzo cha mapato ya Serikali yatokanayo na shughuli za Utalii hivyo ni muhimu kulindwa na kuhifadhiwa kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Dkt. Chana ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kutangaza vivutio vya Utalii kupitia filamu ya The Royal tour inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karubuni.

Ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi za kutangaza vivutio kwa wadau mbalimbali na kutenga muda kutembelea vivutio hivyo ili kuongeza hamasa ya utalii.

Vilevile Mhe. Waziri ametembelea bonde la Kreta ya Ngorongoro na kufurahishwa na shughuli za uhifadhi zilizochangia ongezeko la Wanyama. “Katika eneo la kreta nimeona Faru zaidi ya 8, Tembo, Nyati, Simba na wanyama aina mbalimbali, naomba tuendelee kutunza, kuhifadhi, kulinda na kudhibiti shughuli ambazo zinaweza kuharibu mazingira na ikolojia katika eneo hili” ameongeza Mhe. Pindi Chana.

Katika hatua nyingine Mhe. Waziri ametembelea sehemu ya barabara ya kutoka Hifadhi ya Ngorongoro hadi Golini ambapo ni mpaka wa Hifadhi ya Serengeti kwa lengo la kukagua ukarabati wa Miundombinu ya barabara utokanao na fedha za maendeleo kwa ustawi wa Taifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali.

Kupitia mpango huo NCAA ilipokea jumla ya shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya ukarabati wa barabara na ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa barabara ambapo ukarabati huo utawezesha barabara kupitika msimu wote wa mwaka na kuongeza tija kwenye shughuli za utalii ndani ya Hifadhi.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Maurus Msuha, pamoja na Viongozi wa NCAA.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akikagua gwaride la heshma alilioandaliwa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa NCAA alipowasili uwanja wa ndege wa Ngorongoro kwa ziara ya kikazi katika eneo hilo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (wa tatu kutoka kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Naibu Kamishna wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka (wa pili kutoka kulia) kuhusu ukarabati wa Barabara ya kutoka eneo la Seneto hadi Golini yenye urefu wa Km 88, wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela (wa pili kulia) Mkurugenzi wa Idara ya Wantamapori Dkt. Mauruce Msuha (kulia) na Naibu Kamshna wa NCAA Huduma za Shirika Bw. Needpeace Wambuya (Kushoto)
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (kulia) akimsikiliza Naibu Kamishna wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka kuhusu juhudi za NCAA katika kuhifadhi, kulinda na kuendeleza shughuli za Utalii zinazofanyika katika Hifadhi ya Ngorongoro
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Wanne kutoka kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela (wa nne kutoka kulia), Viongozi wa NCAA na Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa katika geti la kuingia eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakati wa ziara ya Mhe. Waziri

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akielezea kufurahishwa na juhudi za Uhifadhi, utalii na ukarabati wa Miundombinu ya barabara katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Post a Comment

Previous Post Next Post