Na Mwandishi wetu, NCAA.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo tarehe 7 aprili, 2022 amefanya ziara Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zilizoko Karatu Mkoani Arusha kwa lengo la kukagua shughuli za utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Mhe. Waziri amekutana na Menejimenti ya NCAA na kupokea taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo na baadae kukutana na watumishi kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza nao kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi.
Amewapongeza watumishi wa NCAA kwa kuongeza umahiri, uwajibikaji na uadilifu katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu zilizoko katika hifadhi hiyo.
“Kwa sasa taasisi zetu nne za uhifadhi zinaendeshwa kwa mfumo wa Jeshi lazima tuongeza uadilifu, ukakamavu, uwajibikaji na ushirikiano katika utendaji kazi wetu na kila mtumishi ajitume ili kuongeza na kuvutia Wageni ambao kuja kwao tunaongeza mapato ya Serikali”
Amewaasa watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano, kuongeza ubunifu na kuwa tayari kusaidia Jamii inayowazunguka hasa katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, Mhe. Waziri amepongeza uongozi wa NCAA kwa kuwa wabunifu katika kuongeza mazao ya Utalii ndani ya eneo na kujenga vituo vya uwekezaji ikiwepo jengo la Kitega uchumi lililopo katikati ya Jiji la Arusha.
Naibu Kamishna wa NCAA huduma za Shirika Needpeace Wambuya amemualeza Waziri Chana kuwa NCAA pamoja na kuwa na jengo la Kitega Uchumi Arusha pia taasisi hiyo imejipanga kuongeza mazao mapya ya Utalii ikiwemo Utalii wa Faru, Maputo Joto, Utalii wa kutembea usiku na utalii wa farasi.