Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amewataka Maafisa Utamaduni na Michezo kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa Waziri Mkuu jana Aprili 5, 2022 wakati akifungua kikao kazi cha maafisa hao na kuwataka kutumia utaalaam wao kufanya kazi kwa weledi Katika kuendelea kuwapa furaha watanzania.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Aprili 6, 2022 wakati alipokuwa akimkaribisha Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa kufunga kikao hicho cha siku tatu kilichojadili mambo mbalimbali ya sekta hizo.
“Naomba nendeni mkawe karibu na wananchi pia muwe wanyeyekevu kwa sababu tukiwa karibu na wananchi mambo mengi yatakwenda vizuri” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Akizungumzia kuhusu uwajibikaji amesema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alihusia kila mtu akitekeleza wajibu wake maendeleo ya haraka yanawezekana ambapo ametoa wito, kwa maafisa hao kwenda tufanya mageuzi ya tasnia hizo kwa weledi.
Mhe. Mchengerwa ametumia muda huo kumhakikishia Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa kutekeleza maelekezo yote kwa kushirikiana na wadau wote ikiwa ni pamoja na TAMISEMI.
Amesema kuanzia sasa kila afisa atapimwa kutokana na utendaji wake katika kuratibu.
Pia amesema karibuni atazindua program ya mawasiliano ambayo wadau mbalimbali wa sekta wataweza kuwasiliana moja kwa moja na yeye ili kujadiliana na kupata ufumbuzi wa changamoto.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Saidi Yakubu amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa ambapo mada mbalimbali zilijadiliwa.
Amezitaja mada zilijadiliwa kuwa ni pamoja na mwongozo wa uendeshaji wa matamasha ya utamaduni, uratibu na usimamizi wa matamasha ya Utamaduni katika Halmashauri za Wilaya na Mikoa.
Mada nyingine ni uibuaji na uendelezaji wa vipaji na kuongeza fursa za ajira kupitia sekta za u
Utamaduni, Sanaa na Michezo katika ngazi ya mtaa kwa mtaa.
"Lazima tujipange ili tupeleke timu nyingi katika mashindano ya kimataifa. Twendeni tukafanye mapinduzi kwa pamoja"Amesisitiza Naibu Katibu Mkuu, Yakubu.