WAZIRI JAFO ATAKA MAAFISA MAZINGIRA KUSIMAMIA KAMPENI YA ‘SOMA NA MTI’

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo nchini uliofanyika shule ya sekondari ya Dodoma leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akifafanua jambo kwa washiriki wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo nchini uliofanyika shule ya sekondari ya Dodoma leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.   

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Khamis Hamza Chilo,akielezea umuhimu wa kupanda miti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo nchini uliofanyika shule ya sekondari ya Dodoma leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Seleman Jafo amewaagiza Maafisa Mazingira nchini kusimamia kampeni ya ‘soma na mti’ ambayo lengo lake ni  wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo kupanda  miti zaidi ya milioni 14 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia amesema ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

Akizungumza leo Januari 20,2021,Jijini Dodoma  wakati wa uzinduzi wa kampeni ya  upandaji miti kwa wanafunzi wa shule  na Vyuo nchini iitwayo soma na mti,Waziri Jafo amewaagiza Maafisa Mazingira hao kuisimamia kwa vitendo kampeni hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha miti mingi inapandwa nchini.

Waziri Jafo amesema ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inazitaka kila Halmashauri kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini hivyo kwa upande wa kampeni ya upandaji miti kupitia wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo wamepanga kupanda miti zaidi ya milioni 14.

Amesema lengo ni mwanafunzi ajifunie kwamba yeye amepanda pamoja na kuutunza mti kwa ajili ya utunzaji wa mazingira katika shule na vyuo.

Katika hatua nyingine,Waziri Jafo amesema  ukosefu wa mvua katika siku za hivi karibuni umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuna wajibu wa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko hayo. 

“Mvua ilikuwa inaanza kunyesha kuanzia mwezi wa tisa lakini  leo tuna Januari  lakini mvua haijaanza hii ni kutokana na mabadiliko ya Tabia nchi kiwango cha maji katika mabonde na mito yetu yamepungua pia mgawo wa umeme umerudi kutokana na maji kupungua,”amesema.

Naye,Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anaeshughulikia elimu,David Silinde ameagiza kufufuliwa kwa  Klabu za utunzaji  wa mazingira katika shule pamoja na Maafisa elimu kuisimamia kwa vitendo  kampeni ya soma na mti kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.

“Naziagiza shule zote nchini kuanzisha na kufufua Klabu za mazingira hili ni takwa na wala sio ombi nitahakikisha hili tunalitekeleza,”amesema

Kwa upande wake,Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Khamis Hamza Chilo amesema lengo la kuzindua kampeni hiyo ni kuhami viumbe hai,kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na kufuata matakwa ya sheria hivyo  amewaomba watanzania kutunza mazingira na kwao liwe zoezi endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Antony Mtaka aliwataka wale wenye viwanja vipya kupanda miti mitatu katika viwanja hivyo   ikiwemo wa kivuli na mti mmoja miwili ya matunda huku akidai kwamba agenda ya utunzaji wa mazingira katika Mkoa huo ni endelevu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Deus Seif amesema wapo pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan na kwa upande wa walimu kazi inaendelea.

Naye, mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka  shule ya sekondari Dodoma,Monica Marwa ameiomba Serikali kuchimba kisima katika shule ya Dodoma Sekondari ili wanafunzi waweze kumwagilia miti ambayo itapandwa huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea mazingita wezeshi ya kijifunzia na kusomea.

Post a Comment

Previous Post Next Post