TANZANIA, AUDA NEPAD KUSHIRIKIANA MAENEO MATANO SEKTA YA AFYA

 Na WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya  na Wakala wa Maendeleo wa Umoja wa Afrika (AUDA NEPAD)  wamesaini makubaliano ya ushirikiano kwenye maeneo matano ya afya ikiwa ni pamoja na kuboresha afya ya uzazi  huku Bima ya Afya kwa wote ikiwa ni moja ya mambo yatakayoshugulikiwa. 

Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarahe 19 Oktoba, 2024 ofisi ndogo za Wizara ya Afya, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema AUDA NEPAD wako tayari kutoa kiasi cha Dola Milioni Moja (Tsh: bilioni 2.8), zitakazotumika kwenye maeneo ya ushirikiano.

Waziri Mhagama ameeleza kuwa ushirikiano huo  pia utawezesha kuwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wawili kwa kila mitaa, ambao watasaidia kupambana na magonjwa ya milipuko na kupima magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.

 Ameongeza kuwa  mpaka sasa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeshapata kiasi cha Dola Laki Tatu kwa ajili ya usimamizi wa kutosha wa usalama wa vifaa vya afya.

 "Tunataka kuweka mifumo zaidi ya kusimamia vifaa vya afya na tutahakikisha kwamba malengo yanafikiwa na  tukifanya vizuri bidhaa za afya hazitakuwa na maswali," amefafanua Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesema eneo lingine ni  la afya ya uzazi kwa vijana waliopo shule za sekondari ambapo wamepanga kusaidia ili kuepuka mimba zisizotarajiwa kwa vijana hao na kuboresha vituo vya afya ya uzazi, ili kuokoa maisha ya watoto wachanga.

"Vilevile, tumekubaliana kwa pamoja kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na kutumia akili mnemba katika Sekta ya Afya, hali itakayosaidia wataalamu kushirikiana kwa haraka na minyororo mingi kama dawa, tiba na mengine kufikika kwa urahisi," amesema Waziri Mhagana

Waziri Mhagama ameishukuru AUDA NEPAD ambayo imeiunga mkono Tanzania katika maeneo hayo makubwa matano ya Sekta ya Afya.

Kwa upande wake Afisa  Mtendaji MKuu wa AUDA NEPAD Bi. Nardos Bekele amesema,  wametenga kiasi cha Dola Milioni 100 kwa ajili ya miradi mbalimbali kwenye nchi za Afrika.

"Tunayo furaha tuko hapa kushirikiana nanyi tunaunga mkono mnachofanya, hii itawezesha kukuza uchumi wa Afrika, hivyo kwa   pamoja tunahakikisha kuwa jitihada  zinazofanywa zinaungwa mkono na  kuzaa matunda," amesema Bi. Bekele na kuongeza kuwa AUDA NEPAD itaendelea  kuwekeza   Tanzania  na itaongeza fedha zaidi kama utekelezaji utakuwa ni mzuri.

Aidha Bi. Bekele ametoa pongezi kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na mambo mengi mazuri anayoyafanya chini ya uongozi  wake.



Post a Comment

Previous Post Next Post