Na Mwandishi Wetu,Geita
MPANGO wa kutoa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara nchini umewafikia wanafunzi 110,000 kutoka katika shule za msingi zaidi ya 100 katika mikoa ya Dar es Salaam , Geita,Ruvuma, Dodoma na Visiwani Zanzibar.
Mbali na kupata mafunzo ya usalama barabarani wanafunzi wamekuwa wakishindanishwa kuchoro michoro inayotoa ujumbe unaolenga kuelezea usalama baarabarani na kisha washindi kujinyakulia fedha ambazo zinatolewa na Kamuni ya Puma ambayo ndio anayetoa elimu hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Amend.
Akizungumza leo Oktoba 20,2021 wakati wa utoaji wa zawadi kwa wanafunzi walioshinda katika uchoraji wa michoro ya usalama barabarani kutoka Shule tano za msingi mkoani Geita, Ofisa Usalama ba Mazingira wa Kampuni ya Puma Ambokege Minga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo amesema wanatambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa wanafunzi.
Akifafanua zaidi amesema Puma Energy Tanzania Ltd imetoa zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi walioshinda shindano la michororo ya usalama barabarani kwa mwaka 2020-2021 mkoani Geita na kwamba tukio hilo la utoaji zawadi linahitismisha mradi huo kwa kipindi cha mwaka huu uliofanywa Kampuni ya Puma kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la AMEND.
"Mpango huu kaika Mkoa wa Geita ulihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani katika shule tano na wanafunzi wasiopungua12,000 wamefikiwa pamoja na shindano la uchoraji wa michoro inayo hamasisha usalama barabarani.
Katika utoaji huo uliohudhuriwa pia na maofisa wa ngazi mbalimbali wa Jeshi la Polisi ,Kikosi cha Usalama Barabarani, Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Puma amesema wameamua kuja Geita kwa sababu ya ukuaji wa haraka wa mji huo ambapo shughuli za kijamii na ongezeko la watu na magari ambayo yanahatarisha usalama wa watoto wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.
"Mpaka sasa tumeweza kufundisha jumla wanafunzi zaidi ya12,000.. wa shule za msingi katika shule 5 (Tano) za mji wa Geita na hii ikiwa ni mara ya pili kuendesha mafunzo haya mkoani Geita.Mafunzo haya ya usalama barabarani na uchoraji ni kipaumbele chetu kwa lengo la kuwapa uelewa watoto hususani wa shule za msingi juu ya namna bora ya matumizi ya barabara.
"Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. Tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa waTanzania wengi Zaidi. Mpango huu pia kwa mwaka huu unategemea kufanyika katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma na visiwani Zanzibar.
"Jumla ya shule 20 zimefikiwa kwa mpango huu kwa mwaka 2021. “Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi Zaidi nchi nzima. Mkurugenzi wakampuni ya Puma kupitia mwakilishi wake ameahidi pia kuwa Puma Energy itaendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani ikishirikiana na serikali kupitia jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya watanzania,"amesema..
Kwa upande wake Mkaguzi Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Geita Emmanuel shagaya amewaomba wanafunzi waliopata mafunzo hayo wameombwa kufikisha ujumbe unaohusu usalama barabarani.
"Watoto mkifika nyumbani waiteni wazazi wote wawili kisha kaeni chini na baada ya hapo waambieni baba na mama wazingatie usalama wao wawapo barabarani pamoja na kuzingatia usalama wa wengine, tukifanya hivyo tutakuwa salama na tutapunguza ajali za barabarani zitapungua na kuokoa Taifa.
Amesisitiza elimu ya mafunzo ya usalama barabarani ni muhimu kwani kuwepo kwa shughuli nyingi za kijamii zimechangia ongezeko la ajali,lakini kupitia elimu hiyo ni matumaini yao zitapungua.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kalangalala wilayani Geita Prudence Temba amesisitiza umuhimu wa jamii kuzingatia matumizi sahihi ya barabarani huku akiwaomba wanafunzi kufikisha elimu hiyo kwa wazazi au walezi.
Pia amesema kuna wanafunzi ambao wamekuwa wakipanda bodaboda,hivyo wasikubali kupanda bodaboda bila kuvaa kofia ngumu, amewasisitiza wanafunzi hao wahakikishie wanapopakiwa katika magari na wazazi wao kama hawajafunga mikanda,basi waambie wavae na kuwakumbusha ulazima wa kufuata sheria za barabarani.
"Katika eneo letu la Kalangalala kuna muingiliano mkubwa wa watu, hivyo tunaomba mtusaidie kupaka rangi katika maeneo ya wavuka kwa miguu, alama zimefutika na kusabababisha kutoonekana vizuri.Pia tunatoa ombi kwa Kampuni ya Puma itusaidie kutejengea ukuta wa shule ya Msingi Kalangalala, matofali yapo, hivyo mtusaidie michanga na mambo mengine, wala hatutaki fedha,"amesema.
Mgeni rasmi kutoka Ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Geita amesema Masumbuko Magang'bila amewasukuru Puma kwa kupeleka mafunzo hayo lakini ni vema wakaendelea kutoa elimu hiyo muhimu yenye lengo la kuokoa maisha ya watu."Tunapotoa mafunzo kwa wanafunzi maana yake tunakwenda kupeleka elimu hiyo ngazi ya chini kabisa, wanafunzi ambao tunawaona shuleni wana wazazi na walezi wao ndio sisi."
Pia amesema wamefurahishwa na shindano la michoro kutoa elimu ya usalama barabarani na kubwa zaidi zawadi ya Sh.milioni nne ambayo shule itakayotoa mshindi wa kwanza itatoa hamasa kwa shule kuwa mabalozi wazuri, lakini kwa mwanafunzi atakayeshinda na kushika nafasi ya kwanza kwa uchoraji sh.500,000 itakwenda kuongeza hamasa kwa wanafunzi katika kuchora lakini kuwa balozi wa usalama barabarani yeye na wazazi wake.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili amesema siri ya ushindi wa shindano hilo ni kujamini ,kujituma na kuwapa wanafunzi kutambua namna ya kutumia vipaji vyao na hatimaye wameibuka kidedea na kushinda Sh.Milioni Nne wakati mshindi wa kwanza kutoka shule hiyo ameibuka mshindi kwa kuchukua nafasi ya kwanza na kushinda Sh.500,000.
Mshindi wa kwanza wa mashindano ya kuchora mchoro wa usalama barabarani ni Victoria Michael wa Shule ya Msingi Nguzo mbili,mshindi wa pili ni Zabibu Stanford Shule ya msingi Nyankumbu aliyepata Sh.300,000 na mshindi wa tatu ni Paul Haruna wa shule ya Msingi Nguzo Mbili aliyepata Sh.150,000.
Ofisa Elimu Mkoa wa Geita Masumbuko Magang'bila( wa pili kushoto) akiwa na viongozi kutoka kampuni ya Mafuta ya Puma Ambokege Minga, Shirika la Amend na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Geita Emmanuel Shagaya( kulia) wakiwa makini kutafuta mchoro ambao utatoa mshindi katika shindano la kuchora mchoro wa usalama barabarani .Shindano hilo limeandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania kupitia mpango wake wa kutoa elimu ya usalama barabarani.Shule za msingi tano za Geita zimenufaika na mpango huo
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nguzo mbili wakiwa na mwalimu wao Tunu Mjema( kulia) wakishangalia baada ya shule yao kuibuka mshindi wa jumla katika shindano la kuchora mchoro wa usalama barabarani ambalo limeandaliwa na Kampuni ya mafuta ya Puma .Shule tano za msingi mkoani Geita zimeshiriki shindano hilo pamoja na kunuifaika na mafunzo ya usalama barabarani.
Ofisa Elimu Mkoa wa Geita Masumbuko Magang'bila akifafanua jambo wakati wa utoaji huo wa zawadi kwa wanafunzi walioshinda michoro ya usalama barabaraniDiwani wa Kata ya Kalangalala wilani Geita Prudence Temba akitoa ombi kwa Kampuni ya Puma kusaidia kujenga ukuta wa uzio wa shule ya Msingi Kalangalala
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kalangalala wilayani Geita wakiwa makini kufuatilia majina ya wanafunzi walioshiriki kuchora michoro ya usalama barabarani .Shindano hilo limeandaliwa na kampuni ya Puma kupitia programu ya kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi
Ofisa Usalama na Mazingira wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania Ambokege Minga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo akielezea jambo wakati wa tukio la utoaji zawadi kwa washindi wa michoro ya usalama barabarani
Wawakilishi wa wanafunzi walioibuka kidedea katika shindano la kuchora michoro ya usalama barabarani wakipokea zawadi ya fedha kutoka Kampuni ya Mafuta ya Puma ambayo imekuwa ikiandaa mafunzo ya elimu ya usalama barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Amend
Wanafunzi ambao wameingia 10 bora katika shindano la uchoraji michoro ya usalama barabarani( waliosimama nyuma) wakiwa katika picha na viongozi kutoka taasisi na mashirika mbalimbali walioshuhudia utolewaji wa zawadi kwa washindi