WAZIRI KALEMANI NA WADAU WA MAFUTA WAJADILI BIASHARA YA MAFUTA

 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(katikati), akizungumza na wadau wa mafuta nchini, wakati wa mkutano wa kujadili mambo mbalimbali yanayohusu biashara ya mafuta nchini, kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, na  Mwenyekiti chama cha Wafanyabiashara ya Mafuta nchini ( TAOMAC), Orando Da’ Costa( kushoto) , mkutano huo uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Mei 21, 2021.

 

Baadhi wa wadau wa mafuta nchini wakisikiliza Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa kujadili mambo mbalimbali yanayohusu biashara ya mafuta nchini, uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Mei 21, 2021.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa wakala wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja (PBPA) Erasto Simon, (kushoto), Kaimu Kamishna wa Mafuta na Gesi, Sebastian Shana( pili kushoto) na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Nishati na Maji( EWURA),wakiwasikiliza wadau wa mafuta hawapo pichani wakati mkutano wa kujadili mambo mbalimbali yanayohusu biashara ya mafuta nchini, uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Mei 21, 2021.

……………………………………………………

Na Zuena Msuya, DSM

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Wadau wa Mafuta nchini na kujadiliana mambo kadha yanayohusu biashara hiyo na kuunda timu ya watu kumi itakayofikisha mapendekezo ya wadau hao serikalini, ya namna bora ya watanzania kushiriki katika biashara ya uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Aidha timu hiyo pia itapendekeza njia bora ya uwekaji wa vinasaba katika mafuta nchini ili kudhibiti biashara hiyo: Timu hiyo itafanya kazi hiyo kwa muda wa miezi mitatu.

Majadiliano hayo yalifanyika wakati wa mkutano kati ya Dkt. Kalemani na wadau mafuta kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu biashara ya mafuta nchini, uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Mei 21, 2021, na  kuundwa timu ya watu kumi ya kufikisha mapendekezo ya wadau Serikalini.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, Kaimu Kamishna wa Mafuta na Gesi,  Sebastian Shana na viongozi wengine kutoka wizara hiyo.

Wajumbe wa timu hiyo ni kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Vipimo nchini( TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Matumizi ya Nishati na Maji( EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini( TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja( PBPA), Chama Wafanyabiashara ya Mafuta nchini( TAOMAC) na Chama cha Wamiliki wa vituo vya mafuta Tanzania (TAPSOA). 

Katika Mkutano huo, Dkt. Kalemani aliwaeleza wadau wa mafuta kuwa tokea mwezi Aprili mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa Vipimo nchi (TBS) ndiyo mwenye dhamana ya kuweka vinasaba katika mafuta yote yanayoagizwa na kutumika hapa nchini tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na kampuni ya nje.

Aliweka wazi kuwa kwa sasa Serikali inaangalia njia bora, rahisi ya haraka na gharama nafuu kwa kuweka vinasaba katika kila mafuta yanayoingia na kutumiwa hapa nchini ili kuendelea kuimarisha ubora wa mafuta.

Sambamba na hilo alisema kuwa kwa ufanya hivyo serikali imeokoa fedha nyingi zilizokuwa zikipotea.

Hata hivyo aliendelea kusema kuwa lengo la serikali ni kuimarisha mashirika yake ya ndani na kuwaongezea watanzania uwezo na ujuzi wa kufanya kazi mbaimbali kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wao wadau wa mafuta, waliipongeza serikali kwa hatua yake ya kuitumia TBS katika kuweka vinasaba katika mafuta yanayoingia na kutumika nchini jambo ambalo limepunguza ukiritimba katika kazi hiyo.

Pamoja na mambo mengine, wameomba serikali kuliongezea uwezo shirika hilo, ili liweze kufanya kazi zake kwa ubora wa hali ya juu na ufanisi mkubwa katika kudhibiti viwango na ubora wa mafuta nchini.

Aidha, Dkt. Kalemani aliendelea kuwasisitiza wafanyabiashara ya mafuta nchini kufungua vituo vidogo vya mafuta vijijini ili kusogeza karibu huduma ya nishati hiyo kwa wananchi na kwamba tayari EWURA wamepitia upya kanuni ya biashara ya mafuta na kuifanyia maboresho ili kuruhusu vituo hivyo kujengwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post