WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, DKT.NDUMBARO AELEZEA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII INAVYOPAMBANA NA JANGA LA KORONA KATIKA SEKTA YA UTALII

 Waziri wa Maliasili na Utalii,Dkt.Damas Ndumbaro amesema mashine za kupimia Virusi vya Korona kwa Watalii kwa sasa zimepelekwa na zinatoa huduma kwa watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Arusha ikiwa ni Juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukuza sekta ya utalii kwa kuondoa adha kwa Watalii wanaotembelea Vivutio vya Utalii nchini.



Aidha, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Wadau wa Utalii nchini kuendelea kushikamana ili kukiza sekta ya Utalii katika kipindi kigumu kinachoikabili sekta hiyo kutokana na janga la Virusi vya Korona huku Serikali ikiendelea kufanya jitihada za kuendelea kupambana na ugonjwa huo.



Akizungumza na Vyombo vya habari jana Jijini Dar es Salaam, Waziri Dkt.Ndumbaro amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara yaAfya...itaendelea kusogeza huduma hizo ikiwa ni jitihada mahsusi za kukabiliana na ugonjwa huo kwa lengo la kukuza sekta ya utalii nchini.

Amezitaja Jitihada hizo kuwa kwa sasa Watalii wataweza kupata huduma za vipimo vya Korona katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo awali huduma hiyo ilikuwa ikipatikana jijini Dar es Salaam pekee.

Amefafanua kuwa Watalii wanaotembelea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti watakuwa wakipatiwa vipimo vya ugonjwa huo baada ya hapo wanaendelea kutalii huku wakisubiria majibu ya vipimo vyao wakati hapo awali watalii hao walilazimika kukaa Dar es Salaam hadi pale majibu vya vipimo vitoke ndipo waweze kuanza kutalii

Pia, Dkt.Ndumbaro amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa upande wa Arusha imepeleka mashine ya kupimia Virusi vya Korona kwa lengo la kuwawezesha Watalii wote kupata huduma ya kupima virusi vya Korona ambapo hapo awali huduma hiyo ilikuwa ikitolewa Jijini Dar es Salaam pekee

Amesema mashine hizo mbili za kupimia Virusi vya Korona zilizopelekwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Jijini Arusha ni jitihada za Wizara hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Wizara ya Afya... kwa lengo la kuwaondolea usumbufu Watalii kwa kukaa muda mrefu Jijini Dar es Salaam wakiwa wanasubiria kupatiwa majibu yao.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amempongeza Rais wa Tanzania, Mhe.Samiah Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kutaka kuunda timu ya kuchunguza kwa namna gani Serikali inaweza kukabiliana zaidi na na ugonjwa huu hasa kipindi hiki cha msimu wa Utalii unaokaribia.

Dkt.Ndumbaro ametoa wito kwa Wadau kuendelea kuufuata mwongozo wa Kujikinga na Virusi vya Korona uliotolewa mwaka jana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Afya  kwa lengola kukabiliana na ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine, Dkt.Damas Ndumbaro amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuchukua juhudi za makusudi katika kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo nchini ambapo hivi karibuni jumla ya Watalii 15 waliwasili nchini wakitokea nchini Israeli.

Ameongeza kuwa Mwezi Mei mwaka huu Wizara inatarajia kupokea kundi lingine kubwa la Watalii wakitokea nchini Israel.

" Tunapambana usiku na mchana katika kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopon nchini katika katika nchi nyingi Duniani ili tuweze kupata Watalii wengi zaidi" alisisitiza Dkt.Ndumbaro

Akizungumzia athari za ugonjwa wa Korona katika Sekta ya Utalii nchini, Dkt.Ndumbaro amesema Tanzania imepata ahueni kubwa ambapo licha ya tishio la ugonjwa huo lakini imeendelea kupokea idadi ya kuridhisha ya Watalii kutokana na kulegeza masharti ugonjwa huo.

" Ukiona sisi Utalii umeshuka kwa zaidi ya asilimia 50 kwa Wenzetu huko hali ni mbaya sana kwa sababu Watalii wengi ni Wasafiri wa kutoka nchi za nje, Nchi nyingi zimefunga mipaka yao, nchi nyingi zimefanya karantini" amesema Dkt. Ndumbaro

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Ndumbaro amewaonya baadhi ya Watanzania kuacha mara moja tabia ya kuhusisha kila kifo kinachotokea kuwa kimetokana na ugonjwa wa Korona kuposti kwenye mitandao ya Kijamii, amesema hali hiyo imekuwa ikiharibu taswira ya nchi kwa kuonesha kuwa vifo vingi vinesababishws na Korona wakati sio kweli.

  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na vyombo vya habari jana Jijini Dar es salaam kuwa  mashine za kupimia Virusi vya Korona kwa  Watalii kwa sasa zimepelekwa  katika  Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Arusha ikiwa ni Juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukuza sekta ya utalii kwa kuondoa adha kwa Watalii wanaotembelea Vivutio vya Utalii nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Allan Kijazi mara baada ya kuwasili Jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kuzungumza na Vyombo vya habari jinsi inavyochukua hatua katika kupambana na Ugonjwa virusi vya Corona ambao umeathiri sekta ya utalii nchini kwa zaidi y asilimia 50 ambao Wizara katika kukabiliana nao imepeleka mashine mbili kwa ajili ya kuwapimia Watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Arusha

Post a Comment

Previous Post Next Post