WALIMU WASHAURIWA KUITUMIA TSC KUTATUA KERO ZAO

 

Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape akitoa hotuba yake kwenye kikao cha Walimu wa shule za msingi na sekondari wa Wilaya ya Same. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa shule ya sekondari Same na kililenga kuwaelimisha walimu juu ya sheria na taratibu za Utumishi wa Walimu. 

Baadhi ya walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same wakiwa katika hali ya furaha wakati wa kikao kilichowakutanisha na Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC. 

Baadhi ya walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same waliohudhuria kikao kazi wakiwa katika hali ya utulivu wakati kikao kikiwa kinaendelea. 

Mmoja wa walimu akichangia mada wakati wa kikao cha Walimu. 

Mmoja wa walimu akichangia mada wakati wa kikao cha Walimu.

********************************

Na Adili Mhina.

Walimu wametakiwa kuzitumia kikamilifu ofisi za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa kuwasilisha kero na changamoto za kiutumishi wanazokutana nazo katika maeneo ya kazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka na kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Christina Hape wakati wa kikao kazi kilichowahusisha walimu wa shule za msingi na sekondari wa Wilaya ya Same.

Kikao hicho kililenga kutoa elimu kwa walimu juu ya masuala ya ajira, maadili na maendeleo ya utumishi wa walimu, kusikiliza changamoto za walimu pamoja na kupata maoni ya walimu juu ya mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha utumishi wa walimu nchini.

Hape alieleza kuwa serikali iliamua kuanzisha TSC kwa lengo la kumsaidia mwalimu kutatua kero mbalimbali na kufanya mwalimu aweze kutekeleza majukumu yake ya kufundisha wanafunzi katika mazingira ya amani na utulivu.

 “TSC ipo kwasababu walimu mpo, tunafanya kazi kwa kuwa ninyi mpo, sisi ni watumishi wenu na tunawajibu wa kuhakikisha uwepo wetu unawasaidia ninyi kufanya kazi zenu kwa ufanisi. Tupo kwa ajili ya kufanya walimu wafanye kazi kwa furaha na amani”, alisema.

Alifafanua kuwa wapo baadhi ya viongozi wamegeuka kuwa miungu watu na wamekuwa wakiwanyanyasa walimu pale wanapofika kwenye ofisi zao kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria.

“kuna baadhi ya viongozi wakimuona tu mwalimu ameingia ofisini kwakwe hata kabla ya kumsikiliza anaaza kumfokea na kumkaripia mpaka mwalimu anapoteza ujasiri wa kujieleza. Mwingine anagoma kupitisha barua ya mwalimu maksudi tu ili amkomoe mwalimu, bila kuelewa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria”, alisema Hape.

Alisisitiza kuwa mwalimu ni mtumishi wa umma kama walivyo watumishi wa kada zingine, hivyo anastahili kuheshimiwa na kuhudumiwa vizuri sehemu yoyote anapoingia ilimradi hajavunja sheria na taratibu za utumishi wake.

Alieleza kuwa pale ambapo mwalimu amekwenda kwenye ofisi ya umma kwa masuala ya kiutumishi na akaona ametendewa kinyume na utaratibu, asikae kimya, badala yake awasilishe malalamiko kwenye ofisi za TSC ili hatua zichukuliwe kwa haraka na aweze kupatiwa haki yake.

“Mwalimu unapaswa kumheshimu kiongozi wako lakini sio kumuogopa. Miongoni mwa majukumu ya TSC kwa mujibu wa sheria ni kushughulikia malalamiko ya walimu. Hivyo, pale unapotendewa ndivyo sivyo usikae kinyonge, leta malalamiko yako sisi tutawasiliana na mamlaka inayohusika na utapata haki yako”, alisema Hape.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Hape aliwataka walimu wilayani hapo kuhakikisha wanazingatia nguzo za maadili ya kazi ya ualimu ambazo ni pamoja na kumlea mtoto kiakili, kimwili, kiroho na kijamii ili kuandaa taifa la watu wema, wazalendo na walioelimika.

Aliongeza kuwa walimu wanapaswa kusoma na kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayohusu utumishi wa walimu ili kuhakikisha wanafikia malengo ya Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini. 

  

Naye Kaimu Katibu wa TSC Wilaya ya Same, John Limu alieleza kuwa hali ya nidhamu kwa walimu wilayani hapo ni nzuri kutokana na elimu inayotolewa mara kwa mara juu miiko na maadili ya utendaji wa kazi ya ualimu.

“Ndugu Mkurugenzi, hali ya nidhamu kwa walimu wa wilaya hii ni nzuri, katika kipindi cha miezi sita ni shauri moja tu la nidhamu lililofunguliwa. Ukiangalia hata kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwa wilaya hii ni kizuri. Hii ni kwasababu walimu wetu wanajitahidi kufanya kazi kwa nidhamu na weledi”, alisema.

Kwa mujibu wa taarifa ya kaimu katibu msaidizi huyo, Wilaya ya Same ina jumla walimu 1966 wanaofundisha shule za serikali. Katika idadi hiyo, walimu 1150 ni wa shule za msingi na walimu 816 ni wa shule za sekondari.

Post a Comment

Previous Post Next Post