BILIONI 12.6 ZATUMIKA UJENZI WA DARAJA LA MAGARA

 

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimuelekeza jambo Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara Mhandisi Bashiri Rwesingisa (wa kwanza kushoto) wakati akikagua Daraja la Magara katika Barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange.

Sehemu ya Daraja la Magara lenye urefu wa meta 84, lililokamilika kujengwa na Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), kwa gharama ya shilingi bilioni 12.6 kwa kipindi cha miezi 24. Daraja hilo liko kwenye mto Magara eneo la Mwada katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akiongea na baadhi ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini eneo la Haydom, alipopita kukagua barabara ya Mbulu hadi Haydom Kilometa 81 inayoombewa fedha na mbunge wa jimbo hilo ili iweze kujegwa kwa kiwango cha lami.

Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini eneo la Haydom, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), alipopita kukagua barabara ya Mbulu hadi Haydom Kilometa 81, inayoombewa fedha na mbunge wa jimbo hilo ili iweze kujegwa kwa kiwango cha lami.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang Ghaibu Lingo, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akikagua barabara ya Mugitu hadi Haydom Kilometa 68.35 katika eneo la ziwa Basoutu, barabara inayoombewa fedha na Mbunge wa jimbo la Hanang ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. 

………………………………………………………………………..

Ujenzi wa Daraja la Magara lililo umbali wa kilometa 21 kutoka barabara kuu iendayo Arusha eneo la Magara katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu (Kilometa 50.5), mkoani Manyara umekamilika. 

Akikagua daraja hilo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amewaambia waandishi wa habari kuwa ameridhishwa na ujenzi wa Daraja la Magara ambalo ujenzi wake umekamilika ndani ya muda kama ilivyo kwenye mkataba wake. Ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020.

“Serikali ya awamu ya sita itaendelea kusimamia uboreshaji wa miradi miundombinu ya barabara kama ilivyo kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa miradi yote na ahadi zote zitaendelea kutekelezwa na serikali yake ili kuwezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi zitakazopelekea maendeleo kwa taifa letu.” Amesema Mhandisi Kasekenya.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange, ameishukuru serikali kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa Daraja la Magara kwa wakati, ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutawezesha ukuaji wa shughuli za kilimo na ufugaji kwa wananchi wa mkoa wa Manyara na kwamba serikali ya wilaya itahakikisha miundombinu ya daraja la Magara haihujumiwi ili kuilinda thamani ya mradi wa ujenzi wake.

Akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Mhandisi Bashiri Rwesingisa amesema kuwa, mradi wa Ujenzi wa Daraja la Magara lenye urefu wa meta 84, umefanywa na kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG) kwa gharama ya shilingi bilioni 12.6 kwa kipindi cha miezi 24 kwa mujibu wa mkataba wake, kuanzia Februari 2018 hadi Februari 2020 na kwamba kipindi cha matazamio cha mwaka mmoja tayari kimeisha bila tatizo lolote.

Naibu Waziri Kasekenya alikuwa mkoani Manyara kwa ziara ya siku mbili kukagua barabara za Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu Kilometa 50.5, Mbulu hadi Haydom Kilometa 81, Mugitu hadi Haydom Kilometa 68.35 na Singe kwenda Kimotorok hadi Sukuro Kilometa 155, zinazoombewa fedha na wabunge wa Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini, Hanang, Babati Mjini na Babati Vijijini ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post