Walimu Kilolo Waonywa Uhusiano wa Mapenzi na Wanafunzi

 

Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Laini Kamendu juu ya hali ya nidhamu ya walimu katika Wilaya hiyo. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, Kilolo hivi karibuni. 

Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape akitoa hotuba yake kwenye Mkutano wa walimu wa Wilaya ya Kilolo uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilolo, hivi karibuni. Kushoto ni Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Kilolo, Alloys Maira na kulia ni Afisa Mwandamizi kutoka TSC makao makuu, Neema Lemunge. 

Mwalimu Clementina Kilumile wa shule ya msingi Pomerini iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Kilolo, akiuliza swali wakati wa Mkutano uliowakutanisha walimu wa wilaya ya kilolo na Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Christina Hape (hayupo pichani) kutoka TSC makao makuu. 

Mwalimu Daniel Kamwela wa shule ya msingi Ndengisivili iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Kilolo, akiuliza swali wakati wa Mkutano uliowakutanisha walimu wa wilaya ya kilolo na Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Christina Hape (hayupo pichani) kutoka TSC makao makuu.

Baadhi ya walimu wakiwa katika hali ya utulivu wakati wa hotuba ya Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC makao makuu, Christina Hape (hayupo pichani). 

Baadhi ya walimu wakiwa katika hali ya utulivu wakati wa hotuba ya Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC makao makuu, Christina Hape (hayupo pichani).

**********************************

Na Adili Mhina

Walimu wilayani Kilolo wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kujihususha kimapenzi na wanafunzi kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili, kudhalilisha kazi ya ualimu, kuhatarisha ajira na kukatisha ndoto za wanafunzi.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Christina Hape alipofanya mkutano na walimu wa Wilaya hiyo kwa lengo la kutoa elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa walimu.

Katika Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilolo iliyopo wilayani hapo, Hape alieleza kuwa Kilolo ni moja ya Wilaya zenye idadi kubwa ya mashauri ya nidhamu yanayohusu walimu kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanafunzi, jambo ambalo linadhalilisha kazi ya ualimu.

 “Kilolo kuna tatizo kubwa la walimu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi, wote tunatambua kuwa hii ni kuvunja miiko na maadili ya ualimu. Wazazi wametukabidhi watoto ili tuwalee kimwili, kiroho na kiakili lakini baadhi yetu wamewafanya wanafunzi kuwa wapenzi wao, jambo hili halivumiliki,” alisema Hape.

Aliongeza kuwa, kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, wazazi na jamii kwa ujumla inaanza kukosa imani na walimu juu ya usalama wa watoto wao wawapo shuleni, kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Alisisitiza kuwa, moja ya njia za kutokomeza tatizo hilo ni kuhakikisha kila mwalimu anakuwa mlinzi wa mwenzake ili pale inapotokea kuna mmoja anajihusisha na vitendo hivyo, taarifa itolewe mara moja na hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka.

“Ni lazima sasa kila mmoja wetu ajitahidi kulinda hadhi na heshima ya mwalimu, tusikubali kudharaulika kwa sababu ya watu wachache. Kila mwalimu awe mlinzi kwa mwenzake, ukiona kuna mwenzako anafanya vitendo hivyo, toa taarifa kwa mkuu wa shule, kama hachukui hatua nenda ngazi inayaofuata hadi pale hatua zitakapochukuliwa”, alisema Hape.

Aliongeza kuwa TSC haipo kwa ajili ya kuwafukuza kazi walimu, ndiyo maana wakati wote imekuwa mstari wa mbele kuwaelimisha walimu juu ya kanuni na taratibu za utumishi wao ili wasijiingize kwenye makosa ya kinidhamu yanayoweza kukatisha ajira zao.

“TSC tunawapenda sana walimu, hatupendi hata mwalimu mmoja apoteze ajira yake. Wote tunajua kuwa walimu waliopo bado ni wachache, tukiwafukuza tatizo la upungufu wa walimu linaongezeka, lakini pamoja na hayo, hatuwezi kuwafumbia macho walimu ambao hawataki kubadilika, hao lazima tuwaondoe,” alisema.

Kabla ya kufanya mkutano na walimu, Mkurugenzi Hape alifanya mazungumzo mafupi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Laini Kamendu ambaye alikiri kukithiri kwa tatizo hilo kwenye halmashauri yake.

Kamendu alieleza kuwa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa lipo maeneo ya vijijini ambapo wananchi bado hawajawa na mwamko mkubwa katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo visivyofaa ikiwemo vya walimu kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanafunzi.

Aliongeza kuwa kutokana na ugumu wa maisha ya vijijini, baadhi ya walimu wasiozingatia maadili ya kazi yao wanatumia mwanya huo kuwarubuni wanafunzi kwa vitu vidogo vidogo na hatimaye wanawageuza kuwa wapenzi wao.

“Watoto wengi wanaofanyiwa vitendo hivyo wapo maeneo ya vijijini, kwa mfano, kuna eneo linaitwa Itonya, huko hata pikipiki kufika ni shida. Wanafunzi kule hawana uelewa wa mambo mengi kutokana na mazingira, kule mwalimu anaonekana ndiyo kila kitu, chochote atakachotaka mwanafunzi atakubali na matokeo yake ndoto zao zinazimwa”, alisema Kamendu.

Alieleza kuwa ofisi yake imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasilisha taarifa za walimu wenye uhusiano wa mapenzi na wanafunzi kwenye ofisi za TSC wilayani hapo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kama sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2015 inavyoelekeza.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alishauri TSC kutoa mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana ili ikiwezekana afanye marekebisho ya kanuni za sheria hiyo ili kutotoa mwanya wa kuwaachia huru walimu wanaofanya vitendo vya mapenzi na wanafunzi kwa kisingizio cha kukosa ushahidi wa moja kwa moja.

“Kwa kweli kwa hatua tulizochukua, tatizo la walimu kujihusha na mapenzi na wanafunzi limepungua sana. Kinachonisikitisha ni kwamba TSC ngazi ya Wilaya inawafukuza kazi walimu hawa lakini wanapokata rufaa makao makuu wanashinda na wanarudishwa kazini. Tunaambiwa eti hakuna ushahidi wa kutosha, lakini huko mtaani kila mtu anajua hao walimu ni tatizo kwa wanafunzi. Ni vyema mwangalie upya kanuni hizo ili tuwasaidie watoto”, alisisitiza Kamendu.

Hape alimweleza Kamendu kuwa TSC imeona changamoto hiyo na ipo kwenye utaratibu wa kutoa mapendekezo ya kumshauri waziri mwenye dhamana ili kufanya maboresho ya kanuni hizo na kuziba mianya inayowawezesha watuhumiwa kuwarubuni mashahidi ili wasipatikane na hatia.

Post a Comment

Previous Post Next Post