NAIBU WAZIRI AWAPONGEZA TANROADS MANYARA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya (kushoto) akikagua barabara ya Singe-Kimotorok baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Manyara, ambapo ametembelea Wilaya za Babati, Mbulu na Hanang’, kulia ni Meneja wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa
Meneja wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa akisoma taaarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya.
……………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Manyara
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameipongeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoani Manyara kwa namna wanavyotunza, kukarabati na kutengeneza barabara za eneo hilo.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Manyara, Mhandisi Kasekenya amempongeza Meneja wa TANROADS Mkoani Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa.
Amesema anakiri kukutana na wabunge wa mkoa wa Manyara na wameridhishwa na namna TANROADS Manyara wanavyozihudumia barabara zilizopo chini yao na yeye binafsi amejionea hali halisi.
“Wabunge ni wanasiasa na wanaposifia jambo ni kweli kuna kazi imefanyika hivyo nawapongeza TANROADS Manyara kwa namna mnavyofanya kazi hadi wabunge wa mkoa wenu wanawapongeza,” amesema mhandisi Kasekenya.
Amesema katika ziara yake ya siku mbili ametembelea daraja la Magara linalounganisha Wilaya za Babati na Mbulu, barabara ya Mbulu-Haydom, barabara ya Haydom-Mogitu Wilayani Hanang’ na barabara ya Singe Babati-Kimotorok wilayani Simanjiro inayofika hadi wilayani Kiteto.
“TANROADS Manyara nawapongeza mno, kwa namna mnavyotekeleza wajibu wenu katika kuhudumia barabara zote za mkoa mnazozisimamia, hongereni sana,” amesema mhandisi Kasekenya.
Hata hivyo, Meneja wa TANROADS Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo amesema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa kokoto kwa makandarasi wanaotengeneza barabara.
Mhandisi Rwesingisa amesema kutokana na uhaba wa kokoto hizo inawalazimu makandarasi kuzisafirisha kutoka Mkoani Mwanza au Wilayani Bukoba mkoani Kagera.
Ametaja changamoto nyingine ni ukosefu wa wakandarasi wenye uwezo wa kazi za madaraja, hali inayosababisha baadhi ya makandarasi kuikimbia miradi.

Post a Comment

Previous Post Next Post