Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam kupitia Mkoa wa kihuduma Ubungo inatekeleza mradi wa maji Katika eneo la Kimara Golani na maeneo ya Saranga ambao utanufaisha kaya takribani 4000 katika maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa DAWASA Ubungo Bw. Gilbert Massawe ambapo amesema kwa sasa tayari bomba za inchi 8, 10 na 12 zilimelezwa kwa umbali wa kilomita 7.3 pamoja ufungaji wa vitoleo hewa (Air valve) kwenye maeneo matano yenye miinuko katika mradi huo.
"Mradi huu tunaotekeleza unatokana na maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Waziri wa Maji katika kikao cha wananchi kilichofanyika eneo la Golani ambapo kupitia mradi huu wakazi wa Kimara Golani na maeneo ya Saranga yanaenda kuondolewa adha ya ukosefu wa maji kwa asilimia 100%" alisema Massawe.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu ameishukuru DAWASA kwa kufanikisha mradi wa maji wa Golani utakaoweza kuwanufaisha wananchi wa maeneo ya Jimbo lake hasa katika Kata ya Golani pamoja na vitongoji vyake.
Mamlaka imeendelea kusogeza huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam haswa ya Pembezoni yaliyokuwa na changamoto kubwa ili kufikia mwaka 2024 jiji la Dar es Salaam upatikanaji wake wa maji uwe asilimia 100%.
Mbunge wa Kibamba Mhe. Issa Mtemvu akipata maelezo ya utekelezaji wa mradi wa maji Golani kutoka kwa meneja wa mkoa wa DAWASA Ubungo Gilbert Massawe(wa pili kulia) unaotekelezwa na DAWASA kupitia fedha za ndani, ambapo umehusisha ulazaji wa mabomba ya inchi 8, 10 na 12 kwa umbali wa Kilomita 7.3 na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 95. Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha kaya takribani 4000 katika eneo la Kimara Golani na maeneo ya Saranga.Ziara ikiendelea
Meneja wa DAWASA mkoa wa Ubungo Gilbert Massawe akizungumza na wananchi wa mtaa wa Ukombozi Kata ya Saranga
Mbunge wa Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu akiwatoa hofu wananchi wa mtaa wa Ukombozi kata ya Saranga.