MAKANDARASI WAZAWA WATAKIWA KUWA MABALOZI WEMA

  Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amewataka Makandarasi wazawa wote nchini kuwa mabalozi wema kwa kufanya kazi nzuri zinazozingatia viwango na kukamilisha miradi kwa wakati ili Serikali ipate thamani ya fedha katika miradi yote.

Agizo hilo amelitoa mkoani Mwanza katika mkutano wa kwanza wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2023, kanda ya ziwa mkoani humo, ambapo wenye kaulimbiu inayosema “Kujenga Uwezo wa Makandarasi wa Ndani; Mafanikio
na Changamoto”. "Ni muhimu kwenu Makandarasi kuzingatia uzalendo katika shughuli za kikandarasi pamoja na kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya ubora kulingana na mikataba ili wananchi waweze kupata huduma bora kwa wakati na thamani ya fedha iliyokusudiwa"amesema Naibu Waziri huyo.

Kasekenya ameitaka Bodi ya CRB kusimamia kwa vitendo suala la maadili ya taaluma yao kwa kuwachukulia hatua kali Makandarasi wote wanaothibitika kukiuka wajibu wao.

Kasekenya amefafanua kuwa makandarasi wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi yetu na endapo pale makandarasi wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wanawachelewesha wananchi kupata huduma zinazokuwa zimekusudiwa na pia wanaitia Serikali hasara.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya CRB kwa mwaka 2022, Eng. Rhoben Nkori ameeleza kuwa Bodi ilisajili jumla ya makandarasi 1,341 na hivyo kufanya idadi ya makandarasi waliosajiliwa kufikia 14,034. Aidha, Bodi ya CRB imewafutia usajili jumla ya Makandarasi 520 waliobainika kutokujihusisha kikamilifu na shughuli za ukandarasi kwa muda mrefu.

Eng. Nkori amemshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake na kusikia kilio cha makandarasi hususan kuhusu changamoto ya upungufu wa kazi kwa makandarasi wa majengo.

"Kwa namna ya pekee niishukuru Serikali ya Awamu Sita tumeanza kuona ongezeko la kazi za majengo ya Serikali na Taasisi zake zikitolewa kwa wingi kwa makandarasi na tunaamini hawataangusha kwenye ubora na ufanisi", ameeleza Eng. Nkori.

Amefafanua kuwa Bodi imesajili miradi 4,013 yenye thamani ya Trilioni 6.128 ambapo asilimia 50.1 ya thamani hiyo ilitekelezwa na makandarasi wa ndani na asilimia 49.9 ilitekelezwa na makandarasi wageni.

Eng. Nkori ameongeza kuwa Mkutano huu wa mashauriano hapo Mwanza ni wa kwanza kwa mwaka huu kati ya mikutano minne itakayofanyika kikanda, yaani kanda ya ziwa hapa Mwanza, kanda ya nyanda za juu kusini utakaofanyika Mbeya, kanda ya Kaskazini, utakaofanyika Arusha na kanda ya Mashariki utakaofanyika Dar es Salaam.

Mkutano wa mashauriano huo umelenge wadau wa sekta ya ujenzi kutoka Serikalini na sekta binafsi wakiwemo waajiri, makandarasi, wataalam washauri kwa ajili ya kupeana taarifa, kushauriana, kujitathimini, kujisahihisha na kuweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuboresha ufanisi katika shughuli za ujenzi hapa nchini.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa wajumbe walioshiriki mkutano wa kwanza wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2023, Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Eng. Rhoben Nkori, akielezea utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo katika mkutano wa kwanza wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2023, Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.
Baadhi ya washiriki ambao ni makandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, katika mkutano wa kwanza wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2023, Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.



Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akiwa katika picha ya pamoja na makandarasi na Wadau wa Sekta ya Ujenzi mara baada ya kufungua mkutano wa Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kwa Mwaka 2023, Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.

Post a Comment

Previous Post Next Post