Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua namna Taasisi ya Wakala ya vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) inavyopaswa kufanya kazi zake, wakati akifungua Mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo (03.03.2021) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa akitoa neno la shukrani kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) muda mfupi baada ya Prof. Ole Gabriel kufungua Mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Wakala ya vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) uliofanyika leo (03.03.2021) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakala ya vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene akitoa taarifa ya utangulizi kuhusu taasisi hiyo muda mfupi kabla ya kufunguliwa kwa mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo (03.03.2021) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Taasisi ya Wakala ya vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) wakisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo (03.03.2021) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (mbele, katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika leo (03.03.2021) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa na kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakala ya vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene.
***********************************
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Wakala ya Vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuzingatia maadili na uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yakeikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatenda haki ndani na nje ya taasisi hiyo.
Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa Baraza la nane la wafanyakazi wa Taasisi hiyo ambapo ameupongeza utaratibu huo wa kukutana mara kwa mara kwa baraza la wafanyakazi wa taasisi hiyo huku akisisitiza kuwa mikutano hiyo inapaswa kuwa na tija kwa watumishi na watu wote wanaonufaika na uwepo wa taasisi hiyo.
“Mkutano huu ni mkubwa sana na una heshima yake hivyo ni vizuri utumike kujadili kwa kina namna ya kupunguza na kuondoa changamoto za watumishi wa kampasi zote za LITA ili ziweze kutekeleza vyema jukumu la kuzalisha wataalam wa tasnia ya ufugaji hapa nchini” Alisisitiza Prof. Ole Gabriel.
Aidha Prof. Ole Gabriel amatoa wito kwa kampasi zote za taasisi hiyo kuhakikisha zinabadilisha mifumo yake ya ufundishaji ili kuwafanya wahitimu wa vyuo hivyo kuweza kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa kama ilivyozoeleka hivi sasa.
“Huwa inanisikitisha sana kumuona mzazi anamgharamia mwanae ada ya masomo kwa miaka isiyopungua mitatu afu baadae mzazi huyo huyo anaanza kuwajibika kumtafutia mtoto wake ajira, ni lazima tubadilishe huu mtazamo na kwa sababu chuo chenu kimejikita zaidi kwenye vitendo ni wakati sasa mzalishe wataalam watakaojitegemea kwenye soko la ajira” Aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Prof. Ole Gabriel alihitimisha hotuba yake kwa kuitaka LITA kuhakikisha inazingatia usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi wanawake katika ngazi mbalimbali wanazostahili.
“Kuwa mnene au mwembamba ni juhudi za mtu binafsi lakini kuwa mwanamke au mwanaume ni uamuzi wa Mungu hivyo ni si vyema kushindwa kumpa mtu nafasi kisa ni mwanamke na kufanya hivyo kwa kweli ni kosa kubwa sana” Alisema Prof. Ole Gabriel.
Awali akitoa taarifa ya utangulizi kuhusu mafanikio ya Wakala ya Vyuo vya mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa katika kipindi cha mwaka uliopita taasisi hiyo imefanikiwa kuongeza nafasi ya udahili wa wanafunzi kutoka 2536 hadi wanafunzi 3574 mwaka huu.
“Hata hivyo kutokana na ongezeko hilo, tumekuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na mabweni, madarasa, maabara, maktaba na walimu wa fani za afya ya Mifugo na uhandisi kilimo ambapo mpaka sasa tunahitaji walimu 34” Aliongeza Dkt. Mwambene.
Aidha Dkt. Mwambene alibainisha juu ya uwepo wa changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na majengo ambayo kwa sehemu kubwa yanatakiwa kuvunjwa na kujengwa mengine.
“Mhe. Katibu Mkuu, fedha za kuendesha shughuli mbalimbali za vyuo tutapambana tujihudumie wenyewe ila tunaomba Wizara itusaidie tupate fedha za maendeleo kwa ajili ya kujenga miundombinu hii kwa sababu imeshakuwa ya muda mrefu mno, yapo majengo yana zaidi ya miaka 80.” Alisisitiza Dkt. Mwambene.