MANISPAA YA MOSHI IWE MFANO WA KUIGWA KATIKA UTUNZAJI WA MAZINGIRA-WAITARA

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mwita Waitara akiwa katika ukaguzi wa mazingira katika soko la Tandika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mwita Waitara baada ya kuwasili katika soko la Tandika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mwita Waitara akikagua Machinjio ya Ngombe ya Mbagala yaliopo Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

*************************************

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mwita Waitara amesema kuwa Manispaa ya Moshi iwe mfano wa kuigwa katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira ameeleza kuwa Manispaa ya moshi imejitahidi sana katika kudhibiti taka ngumu hivyo Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam zitumie mbinu ambazo zitaweza kudhibidi uchafuzi wa mazingira kama Manispaa ya Moshi.

Ameyasema hayo alipokuwa katika ukaguzi wa mazingira katika Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam.  Alisema kuwa kuna haja ya kila Manispaa kuchukua hatua ya kuhakikisha Manispaa yake inakuwa safi kwa kuzingatia udhibiti wa taka ngumu na maji taka yanayotoka vyooni.

“Mtu hawezi kumiliki Gesti au Bar alafu hana choo, hii ipo kinyume ya sheria. Endapo utakuta mtu anamiliki Gesti na hana choo apigwe faini na endapo atashindwa kutekeleza masharti aliyopewa adhabu iongezwe ili kuepusha uchafuzi wa mazingira na usalama wa kiafya kwa wananchi. Kuna utaratibu wa watu kufungulia vyoo vyao kipindi cha mvua na kusababisha harufu mbaya na usalama wa Raia kuwa hatarini. Hivyo naagiza Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam kusimamia swala hilo na kuchukua hatua kwa wale wote wanaochafua mazingira kwa kufungulia vyoo kipindi cha mvua”

Aidha Mhe. Waitara ametembelea soko la Tandika na Machinjio ya Ng’ombe ya Mbagala Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kujionea hali halisi ya kimazingira katika maeneo hayo. Akiwa katika Machinjio ya Ng’ombe, Mhe. Waitara ameeleza kuwa Manispaa ya Temeke haina machinjio binafsi ambayo yanamilikiwa na Serikali bali wananchi wanapata huduma kutoka machinjio ya mtu binafsi lakini pamoja na kutoa huduma kwa wananchi amebaini eneo hilo linahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa.

“Kwakuwa hakuna machinjio ya Serikali mmiliki wa machinjio anahitaji kupewa ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha anafanya shughuli zake bila kuchafua mazingira na kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokaa karibu na machinjio haya. Naagiza wataalamu kutoka Manispaa ya Temeke, NEMC na Bonde waje katika machinjio haya kukagua, kupima maji yaliyo karibu na machinjio na kutoa ushauri wa kitaalamu” Mhe. Waitara alisema.

Vilevile Mhe. Waitara ametembelea soko la Tandika na kubaini changamoto nyingi za kimazingira zinazowakabili wafanya biashara katika soko hilo. Kutokana na malalamiko ya wananchi juu ya maji machafu yanayotiririka yenye harufu mbaya kutoka kwenye machinjio ya kuku ya soko, Mhe. Waitara amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuhakikisha mtaro unaozunguka soko unasafishwa na

maji machafu yanayotiririka ambayo sio salama kwa wafanya biashara wa eneo hilo yaondolewe mara moja.

“Soko ni chanzo cha mapato ya Manispaa na wananchi wanalipa kodi kwa maendeleo ya Taifa hivyo kunahaja ya kuwasimamia na kuhakikisha mazingira yao yanakuwa salama kwa afya zao. Nashukuru Mhe. Mkuu wa Wilaya yupo hapa atasimamia mkae nyie wafanyabiashara, uongozi wa Manispaa ya Temeke na uongozi wa soko ili mkubaliane namna ya kusimamia usafi katika soko hili.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe amesema kuwa amefurahishwa na ujio wa Naibu waziri na kuweza kutembelea maeneo ya soko kujionea mazingira kwa hii imekuwa chachu kwa Manispaa ya Kinondoni

“Nakuahidi Mhe. Naibu Waziri nitashirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuhakikisha changamoto zilizojitokeza zanafanyiwa kazi kwa wakati na ukamilifu ili kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa safi na salama. Nitahakikisha tunafanya kikao na wadau wa soko ili kutatua changamoto hizo” Mhe. Gondwe.

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke Mhe. Doroth Kilave amesema kuwa changamoto zipo lakini tutahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa kwa wakati kwani kuzungumza na wananchi inasaidia kufahamu changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Naye Kaimu Meneja wa Mashariki Kusini – Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Taimul Kisiwa, amesema kuwa ziara ya Mhe. Naibu Waziri imeenda vizuri na maelekezo yameshatolewa lakini elimu juu ya maswala ya utunzaji wa mazingira inahitajika kwani wananchi wengi hawajui kama wao pia ni wahusika wakuu katika utunzaji wa mazingira wanajua serikali tu ndio inawajibu wa kusimamia mazingira.

Naibu Waziri Mhe. Waitara yuko katika ziara ya siku tano katika Mkoa wa Dar es Salaam kujionea hali halisi ya kimazingira katika mkoa huo. Ameshatembelea Manispaa ya Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke.

Post a Comment

Previous Post Next Post