*****************************************
NA VICTOR MAKINDA. MOROGORO
Tanzania imepata mafaniko makubwa kwa kuwa na vivutio bora zaidi vya utalii duniani ambapo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, imepigiwa kura na kushinda kuwa mbuga bora zaidi ya hifadhi ya wanyamapori duniani.
Hayo yamesema mapema leo mjini Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbalo, katika maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani yaliyokwenda sambamba na mkutano wa wadau wa sekta ya utalii.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Ndumbalo alisema Tanzania imeshinda tuzo hiyo na kuwa ya kwanza kupitia hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mlima Kilimanjaro zikiwa zimeshika nafasi za juu katika tuzo hizo ambazo hutolewa na taasisi ya Chief Traveler Award (CTA).
“Yalichaguliwa maeneo 25 yanayovutia zaidi kwa utalii kote duniani, katika hayo maeneo matatu yametoka Tanzania, ambapo eneo la kwanza lililopigiwa kura na kushinda kwa kuwa kivutio cha kwanza bora zaidi duniani ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na Tarangire zikiwa ni miongozi mwa maeneo bora zaidi vivutio vya utalii.” Alisema Dkt Ndumbalo.
Dkt Ndumbalo alisema kuwa mafaniko hayo hayakuja tu bali yametoka na mikakati ya dhati ya serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi shupavu wa Rais John Magufuli, katika uwekezaji na usimamizi madhubuti wa hifadhi zetu za Taifa.
Dkt. Ndumbalo alitoa wito kwa watanzania, kujivunia mafanikio hayo huku wakifanya kila linalowezekana kuvitangaza vivutio hivyo vya utalii mahali pote duniani kwa lengo la kuzidi kukuza utalii na kuueleza ukweli Ulimwengu juu ya ubora wa vivutio vilivyopo nchini kwetu.
Katika hatua nyingine Dkt Ndumbalo, alisema kuwa kiwango cha ujangiri kwa wanyamapori na mazao ya misitu kimepungu na kufika asilimia 90, ambapo aliwawaonya watu wote wanaofanya shughuli za kibiniadamu maeneo ya hifadhi, ikiwa ni kilimo au ufugaji, kuacha mara moja kwani serikali itakapowabaini itawachukulia hatua kali za kisheria.
“Sisi kama Wizara tumejipanga, tukimkamata jangiri halali yetu, ama zake ama zetu. Itakapohitajika kupiga ngumi, tutapiga ngumi, kupiga katafunua tutapiga katafunia, ili atakayeingia kwenye maeneo ya hifadhi na kutaka kuharibu ikolojia na uhifadhi ashughulikiwe kikamilifu na hatutakuwa na huruma na mtu yeyote. Alisema Dkt Ndumbalo.
Naye Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya siku ya Wanyapori Duniani, alisema kuwa anazishukuru taasisi zote zilizo chini Wizara za Maliasili na Utalii, ikiwemo TAWA na TANAPA kwa ushirikiano mkubwa ambao wanawapatia hususani wakati ambao wanyamapori wanaingia kwenye makazi ya watu.
Loata alisema kuwa mkoa wake utaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuhakikishakuwa misitu, wanyamapori, mabonde oevu na maeneo yote ya akiba na tengefu yanalindwa a kutuzwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.