WATUMISHI WA NISHATI WAFURAHIA KUTEMBELEA MRADI WA JNHPP

 

………………………………………………………………………………………
Na Zuena Msuya, Pwani
Watumishi wa Wizara ya Nishati, wamesema kuwa  wamefurahia  sana ziara ya kutembelea Mradi wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere(JNHPP) Mkoani Pwani.
Ziara hiyo ya Siku tatu imeratibiwa na Uongozi wa Wizara ikisimamiwa na msimamizi wa Mradi huo kutoka Wizara ya Nishati,  Mhandisi Christopher  Bitesigirwe kwa kushirikisha  watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya wizara hiyo.
Wamesema  kuwa ziara hiyo imekuja wakati muafaka na imekuwa na ufanisi mkubwa kwa kuwa  wamejifunza na kujionea hali halisi ya kinachoendelea katika mradi huo.
Watumishi hao wamesema kuwa wanaushukuru sana Uongozi mzima wa Wizara kwa kuridhia na kuwawezesha watumishi  wake kutembelea mradi huo pamoja na yule aliyetoa wazo la watumishi kutembelea mradi huo na waliounga mkono.
” Sisi watumishi  tunajisikia fahari na kujivunia sana kwa  kuwa sehemu ya mradi huu kwa kuuona kwa macho yetu na vitendo,  utekelezaji wake tangu hatua za awali na si kwa maandishi wala kusimuliwa, 
Hakika tutapata cha kueleza vizazi vyetu hapo  baadaye “,  Walisema Watumishi hao.
Watumishi hao walienda mbali zaidi kwa kusema kuwa,  huo ni mwanzo mzuri kwa Wizara yao, na wanaimani  itaendelea kuwashirikisha kwa kuwapa ridhaa ya kutembelea  katika miradi mingine inayoendelea kutekelezwa.
Hata hivyo walieleza kuwa utaratibu huo umeongeza chachu ya kuitendaji kwa watumishi hao kufanya kazi kwa kasi kubwa, Ubunifu, Umakini zaidi na kwa usahihi na kujiona ni sehemu ya Mradi huo.
Ziara hiyo ya Siku tatu inahusisha Watumishi wote wa Wizara ya Nishati kutoka Idara na Vitengo mbalimbali ambao hutembelea mradi huo kwa awamu tofauti na katika Makundi.

Post a Comment

Previous Post Next Post