Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na mgeni rasmi Bw. Gerald Kusaya akihutubia wakulima wa kijiji cha Isele Tarafa ya Pawaga wilaya ya Iringa leo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ghala la kisasa na vifaa vya kuvunia na kuhifadhia mpunga vilivyotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo ( FAO) kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya. Kulia aliyekaa ni Msemaji wa EU nchini Bw. Cedric Merel na Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw Gerald Kusaya akikabidhi cheti pongezi kwa mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji mpunga ya Tungamalenga Bi. Angelika Kasimba wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya kuvunia mpunga vilivyotolewa na FAO leo wilayani Iringa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa ameshika mkasi kukata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa ghala la kisasa la kuhifadhia mpunga kwa wakulima wa kijiji cha Isele wilaya ya Iringa.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela na kushoto ni Msemaji wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya nchini Bw. Cedric Merel .Ghala hilo limejengwa kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na kusimamiwa na FAO.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( alivaa tai) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa mkoa wa Iringa, mashirika ya EU,FAO ,RUDI na wakulima mara baada ya makabidhiano ya ghala la kisasa na vifaa vya kuvunia zao la mpunga kijiji cha Isele wilaya ya Iringa leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( aliyevaa tai kulia) akiwa na mwakilishi wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya nchini Bw. Cedric Merel wakati wa kukabidhi mashine ya kisasa ya kuvunia mpunga kwa wakulima wa kijiji cha Isele wilaya ya Iringa leo.
Msemaji wa EU nchini Bw. Cedric Merel akitoa salamu za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya leo wakati wa halfa ya makabidhiano ya ghala la kisasa na vifaa vya kuvunia mpunga kwa wakulima toka skimu 12 za mkoa wa Iringa iliyofanyika kijiji cha Isele wilaya ya Iringa leo. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya aliyekuwa mgeni rasmi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amepongeza kazi zilizofanywa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kusaidia wakulima zaidi ya 10,000 wa mpunga wa mkoa wa Iringa kuongeza tija na uhifadhi .
Ametoa pongezi hizo leo (10.12.2020) wakati wa hafla ya kukabidhi ghala na vifaa vya kuvunia mpunga kwa wakulima wa skimu 12 za mkoa wa Iringa tukio lililofanyika kijiji cha Isele tarafa ya Pawaga wilayani Iringa.
Katika hotuba yake Katibu Mkuu huyo wa Kilimo alisema serikali inashukuru kwa dhati Umoja wa Ulaya na shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kusaidia jitihada za serikali za kuendeleza sekta ya kilimo nchini ambapo kwa mkoa wa Iringa katika kipindi cha miaka mine toka 2017 hadi sasa wakulima wa mpunga wamenufaika.
“ Tumeshuhudia mradi wa RICE chini ya shirika la RUDI uliofadhiliwa na EU ukiwezesha wakulima wa zao la mpunga kuongeza tija, kupunguza upotevu, kuongeza ushindani wa kibiashara na kusaidia upatikanaji na usalama wa chakula na kuongeza kipato cha wakulima zaidi ya 10,000 wa Iringa wamenufaika “ alisema Kusaya.
Kusaya alikabidhi ghala la kuhifadhia mpunga kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela lililojengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa uratibu wa FAO ambapo litatumika na wakulima wa mpunga wa kijiji cha Isele kuhifadhia mazao yao hali itakayopunguza upotevu na kuongeza uhakika wa masoko.
Uwepo wa ghala hilo utasaidia pia nchi kuwa na usalama wa chakula kwani mazao yatahifadhiwa kwa muda na ziada itauzwa ili kiwawezesha wakulima kupata kipato cha uhakika alisisitiza Kusaya.
Kwa upande wake Msemaji wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Cedric Merel alisema kukamilika kwa ghala hilo la kisasa lenye uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya 500 pamoja na vifaa vya kuvunia mpunga vimegharimu Shilingi Milioni 774.8 zilizotolewa na Umoja wa Ulaya.
Merel aliongeza kusema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 Jumuiya ya Ulaya imesaidia kuendeleza sekta ya kilimo kwa kufadhili miradi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya chai, kahawa, pamba, sukari ,mpunga, maua na mboga mboga ili kusaidia jitihada za serikali kukuza uchumi wa Tanzania.
“Lengo la Jumuiya ya umoja wa Ulaya ni kuhakikisha mazao ya wakulima wanaongeza uzalishaji na kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani ikiwemo mchele badala ya mpunga ili kuwa na uhakika wa kipato waondokane na umasikini” alisema Merel
Mwakilishi huyo wa Kamiseni ya Umoja wa Ulaya aliongeza kusema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mpunga ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa kupunguza Upotevu wa Mazao Baada ya Kuvunwa uliozinduliwa mwaka jana na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan hivyo amewataka wakulima kutumia ghala hilo kwa lengo kusudiwwa.
Akihitimisha salamu za Umoja wa Ulaya Merel alishauri Viongozi wa wilaya ya Iringa kuwasaidia wakulima wa mpunga kufahamu na kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili wawe na uhakika wa kuuza mchele wao kwa bei ya soko na kujiongezea kipato kwa kuepuka walanguzi wa zao hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alishukuru serikali kwa kuwa na uhusiano chanya na jumuiya za kimaitaifa ikiwemo Umoja wa Ulaya na FAO hali iliyopelekea miradi ya kilimo na mingine kupata ufadhili.
Kasesela aliongeza kusema kukabidhiwa ghala hilo la kisasa lililojengwa na FAO kutachochea uhifadhi wa mpunga wa wakulima wa kijiji cha Isele na pia kuongeza uzalishaji wa zao hilo linalotegemewa kwa chakula na biashara na watanzania wengi.
“Tunashukuru FAO kwa kuratibu na kusimamia ujenzi wa ghala hili hapa Isele kwani litatusaidia kutunza mazao ya wakulima na kupunguza tatizo la upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno” alisema Kasesela.
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa onyo kwa wakulima na Viongozi wa kijiji cha Isele na kata ya Mlenge kutotumia ghala hilo kama ukumbi wa mikutano bali wahakikishe wanaongeza uzalishaji wa mpunga na mazao mengine na kuyahifadhi ghalani hapo” alisisitiza Kasesela.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Shirika la Chakula la Umoja na Kilimo wa Mataifa Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo nchini Tanzania Charles Tulahi alisema wakulima wa mpunga wa Iringa watumie uwepo wa ghala hilo na mengine kuhifadhi mazao yao ili yasiharibike kabla ya kufikishwa sokoni ndio maana wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutumia ghala na vifaa vya kisasa vya kuvunia mpunga.
Tulahi alisisitiza kuwa FAO itaendelea kuunga mkono jitihada za wakulima ili kuhakikisha lengo la kupata chakula cha kutosha na kupunguza upotevu wa mazao shambani na baada ya kuvunwa linafanikiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo mazao ya wakulima hupotea kwa kiwango kikubwa kati ya asilimia 30 hadi 40 kila mwaka kutokana na uvunaji mbaya na kutokuwepo miundombinu bora ya kuhifadhi mazao baada ya mavuno