WAZIRI KALEMANI AUTAKA UONGOZI WA WIZARA YA NISHATI KUFANYA KAZI KWA KASI NA UBUNIFU

 

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Leonard Masanja, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato, (hayumo pichani) kwenye kikao cha Menejimenti ya Wizara hiyo kilichofanyika leo kwenye ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Leonard Masanja akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake kwa Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato, ( hawamo pichani) katika mkutano wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati uliofanyika leo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. 
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao cha Menejimenti kilichofanyika leo katika ofisi za Wizara hiyo, zilizopo Mtumba, jijini Dodoma. 
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ofisini kwake leo katika mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma kabla ya kukutana na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati. 
*************************************
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati kufanya kazi kwa kasi na kwa ubunifu ili kuhakikisha sekta ya Nishati inaendelea kukua ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa maendeleo ya Viwanda na kuliletea Taifa maendeleo.
Waziri Kalemani ameyasema hayo leo Desemba 10, 2020 wakati akiwa kwenye kikao na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati kilichofanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Kikao hicho cha Waziri na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Stephen Byabato, kimelenga kutambulisha viongozi wa Wizara hiyo na kutoa maelekezo yanayolenga kuwa na utekelezaji mzuri wa malengo yaliyowekwa katika Sekta ya Nishati.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kalemani ameiagiza Menejimenti ya Wizara hiyo kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika na wa kutosha unazalishwa nchini kutoka kwenye vyanzo vya gharama nafuu hasa maji.
Pia, ameitaka Menejimenti ya Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya kusafirishia umeme kutoka kona zote nne unakamilika kwa wakati na kuwe na mtandao wa njia ya kusambazia umeme kwa kona zote nne kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi.
Vilevile, Waziri Kalemani, ameuagiza uongozi wa Wizara ya Nishati, kuhakikisha kuwa vijiji vyote 2884 ambavyo havijaunganishwa na umeme, ifikapo mwezi Desemba 2022, viwe vimeunganishwa na huduma hiyo.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ameahidi kutoa ushirikiano mzuri na kufanya kazi kwa weledi katika kuhakikisha majukumu ya Waziri wa Nishati yanafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post