BILIONI 1.4 ZATUMIKA KUIMARISHA KITUO CHA UTAFITI WA MICHIKICHI KIHINGA

 

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ( wa pili toka kushoto) akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kulia) wakati walipotembelea kituo cha utafiti wa zao la michikichi Kihinga Manispaa ya Kigoma jana. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikagua kitalu cha miche bora ya michikichi kwenye kituo cha utafiti wa zao la michikichi Kihinga mkoa wa Kigoma jana. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikagua mche bora wa mchikichi aina ya tenera uliotafitiwa na kituo cha utafiti (TARI) Kihinga jana ambapo miche hiyo inagawiwa kwa wakulima.

( Habari na picha na Wizara ya Kilimo) 

*****************************************

Wizara ya Kilimo imefanikiwa kuimarisha shughuli za utafiti wa zao la michikichi kwa kukipatia kituo utafiti cha TARI Kihinga Shilingi Bilioni 1.4 kuzalisha miche ya michikichi na ununuzi wa vitendea kazi vya watafiti.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (17.12.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipotembelea kituo cha utafiti wa zao la michikichi (TARI) Kihinga kukabidhi trekta moja na vifaa vyake kwa ajili ya shughuli za utafiti wa michikichi.

Kusaya alibainisha kuwa tangu kituo cha utafiti wa zao la michikichi kianzishwe mwaka 2019 tayari wizara imefanikiwa kuzalisha mbegu bora na miche ya michikichi milioni nne na laki mbili ambayo imegawiwa kwenye halmashauri za mkoa wa Kigoma.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema lengo la ziara yake ni kufuatilia agizo la serikali la kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa mafuta ya kula yanayotokana na zao la michikichi.

“Tanzania tuna mahitaji ya tani 570,000 za mafuta ya kula wakati uzalishaji wetu umefikia tani 205,000 kwa mwaka hali inayofanya tuwe na upungufu wa takribani tani 365,000 za mafuta ya kula kila mwaka jambo ambalo halikubaliki kutkana na Tanzania kuwa na ardhi nzuri ya kilimo “alibainisha Kusaya.

Kusaya alisema kufuatia hali hiyo serikali imekuwa ikitumia zaidi ya shilingi Bilioni 443 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi wakati tunao uwezo wa kulima mazo ya michikichi, karanga, ufuta, alizeti yenye kutoa mafuta.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kituo cha Utafiti (TARI) Kihinga Dkt. Filson Kagimbo alisema anaishukuru serikali kwa kukipatia kituo hicho Shilingi Bilioni 1.4 zilizowezesha shughuli za utafiti wa mbegu bora za michikichi na kununua vitendea kazi ikiwemo trekta na zana zake.

Dkt. Kagimbo alisema watafiti wataendelea kushirikiana na taasisi za umma na binafsi kuhakikisha lengo la kuzalisha miche milioni tano kwa mwaka linafikiwa na miche hiyo inafikishwa kwa wakulima ili wapande.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geofrey Mkamilo alisema taasisi yake ianendelea kuzalisha mbegu bora ya michikichi aina ya Tenera yenye uwezo wa kuzalisha tani 4 hadi 5 za mafuta ya mawese kwa hekta tofauti na mbegu ya zamani aina ya Dula yenye kuzalisha wastani wa tani 1.6 hadi 2 kwa hekta.

“Tutaendelea kusimamia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha mkoa wa Kigoma unakuwa na mbegu na miche bora ya michikichi kabla hatujaanza kuisambaza mikoa mingine 17 inayolima zao hilo, hivyo tunaomba wakulima kupitia halmashauri waje hapa Kihinga kuchukua miche ya michikichi “alisisitiza Dkt. Mkamilo.

Mkurugenzi huyo mkuu alisema zao la ndilo lenye uwezo wa kutoa mafuta mengi ya kula na kutosheleza Taifa tofauti na mazao mengine ndio maana watafiti wanaendelea kujikita katika kuzalisha mbegu bora nyingi na zenye matokeo mazuri kwa manufaa ya wakulima na taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post