***************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wazalishaji wa Matofali ya Kuchoma wameshauriwa kuzalisha matofali yanayokidhi viwango ili kuweza kuwanufaisha watumiaji na kuepuka madhara yatakayojitokeza.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Afisa Viwango Kitengo cha Ujenzi Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Aziz Abdalah amesema kiwango cha utengenezaji wa matofauli ni cha lazima kwahiyo mzalishaji analazimika kwa mujibu wa sheria kuhakikisha anazalisha matofali yanayokidhi viwango vya ubora.
"Mzalishaji wa matofali ya kuchoma kama amezalisha matofali ambayo hayajakidhi viwango basi kimsingi atakuwa amefanya kosa kwa mujibu wa sheria".Amesema Mhandisi Aziz.
Aidha Mhandisi Aziz amesema kuna uimara wa tofali unatokana na udongo hivyo kuna udongo ambao haufai kwa matumizi ya matofali na pia kuna udongo ambao unafaa kwa matumizi ya matofali
"Kuna changamoto ya tofali kubanduka ile inatokana na udongo uliotumika kuna udongo mwingine unakuta una chumvichumvi sasa zile chumvichumvi zinapokutana na unyevuvyevu, chumvi inatabia ya kufyonza unyevunyevu na kusababisha tofali kubanduka".
Hata hivyo Mhandisi Aziz amesema ili wazalishaji waweze kujiridhisha na ubora wa matofali ambayo wanazalisha wanatakiwa kufika kwenye ofisi za Shirika la Viwango Tanzania na kuweza kuhudumiwa.
Pamoja na hayo Mhandisi Aziz amesema Kiwango cha Matofali ya kuchoma kimeelezea hasa mambo mbalimbali ikiwemo aina ya matofali ambayo yamegawanyika katika makundi manne ambayo ni matofali ya kawaida,Matofali ambayo yanauwezo mdogo wa kufyonza maji,Matofali ambayo yanatumika kwenye uhitaji wa uimara zaidi na Matofali ambayo haitaji muonekano mzuri.