KILIMO MSETO NI UKOMBOZI WA UHAKIKA WA CHAKULA NCHINI-KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( katikati) akikagua akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dkt. Vicent Naano (kushoto) na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Mthapula (kulia) leo alipowasili kwenye viwanja vya maonesho ya Kilimo Mseto mjini Musoma ambapo ameyafungua rasmi.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akijaribu mashine ya asili ya kusaga mazao iliyotengenezwa na wajasiliamali shirika la Mavuno Project ya Karagwe leo alipofungua maonesho ya kilimo mseto mjini Musoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa ameshika kiazi lishe kilichozalishwa na wakulima wa kikundi cha PCI cha Musoma ambao hufanya kazi ya kufundisha mashuleni namna ya kuongeza uhakika wa chakula kupitia kilimo mseto cha mahindi,viazi na maharage.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama miche bora ya mazao ya bustani wakati alipotembelea banda la wakulima toka wilaya ya Ukerewe wakati alipofungua maonesho ya kilimo mseto yanayofanyika Musoma leo. Kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi. Karoline Mthapula.

Sehemu ya washiriki wa maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto wakiingia uwanjani kwa maandamano leo mjini Musoma.

Sehemu ya washiriki wa maonesho ya siku tatu ya kilimo mseto wakiingia uwanjani kwa maandamano leo mjini Musoma.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo) 

………………………………………………………………………………

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya leo amewasili mkoani Mara na kuzindua maonesho ya siku tatu ya kuhamasisha wakulima na wafugaji nchini kutumia kilimo mseto ili kuongeza uhakika wa chakula na kipato.

Maonesho ya Kilimo Mseto yanafanyika mjini Musoma kwa kuwashirikisha wakulima, wafugaji na wavuvi chini ya uratibu wa shirika la Vi Agroforestry pamoja na taasisi za serikali na wadau wa sekta ya kilimo.

” Nimekuja hapa Mara kuwatia moyo wakulima waendelee kujikita katika kilimo mseto kwa kuwa kinafanya vema katika kuhakikisha kaya na taifa linajitosheleza kwa chakula” alisema Kusaya.

 

Kusaya aliongeza kusema wizara ya kilimo inaendelea kujanga mazingira wezeshi kwa wakulima kupata elimu na teknolojia bora ili kilimo kiwe na tija na kukuza uchumi  hivyo uwepo wa maonesho haya una mchango mkubwa kwa wakulima.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mara Kalorine Mthapula amesema mkoa huo unaendelea na kazi ya kuhamasisha wakulima kujikita katika kwenye shughuli za kilimo na kuwa kupitia maonesho ya kilimo mseto wana uhakika uchumi wa mkoa utaendelea kukua.

Katibu Tawala mkoa huyo alieleza kuwa pamoja na maonesho ya kilimo mseto mkoa huo umeanzisha viwanja maalum vya Nanenane vinavyojulikana kama Mama Maria Nyerere wilayani Butiama kwa lengo la kutumika kufanya maonesho ya kilimo,mifugo na uvuvi ii elimu iwafikie wananchi wengi kwa ukaribu.

” Kila tarehe 15 Septemba mkoa wa Mara huadhimisha siku iitwayo Mara Day kwa lengo la kuhamasisha kilimo, mifugo na uvuvi kupitia viwanja vetu vya Nanenane vya Mama Maria Nyerere huko Butiama ambapo pia siku hiyo hutumika kuhamasisha uhifadhi endelevu la bonde la mto Mara” alisema Mthapula.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Vi Agroforetry Thadeus Mbowe alisema maonesho ya mwaka huu yamesheni teknolojia mbalimbali za kilimo mseto kupitia washirika wenza wakiwemo watafiti na wataalam wa kilimo wanaotoa elimu kwa wananchi.

” Lengo kuu la maonesho haya ni kueneza mchango wa kilimo mseto katika kuboresha maisha na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi  na kuendeleza mjadala wa uhitaji wa sera ya Taifa ya kilimo mseto” alisema Mbowe.

Kauli mbiu ya maonesho ya Kilimo mseto mwaka huu inasema ” Kilimo mseto kwa usalama wa chakula na kipato”.

Kilimo mseto ni kilimo kinachopambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoathiri kilimo.

Mwisho

Imeandaliwa na;

 Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MUSOMA

Post a Comment

Previous Post Next Post