WATANZANIA ANZISHENI VIWANDA VYA MBOLEA NCHINI-KM KUSAYA

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kushoto) akiongea na Meneja Ubora wa Kiwanda cha mbolea za asili cha Guavay, Latifa Mafumbi kilichopo Gongolamboto Dar es Salaam alipofanya ziara kukagua uzalishaji mbolea .

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitazama mtambo wa kuchanganya mbolea ya asili ( Organic Fertilizer) wakati alipotembelea kiwanda cha Guavay kilichopo Dar es Salaam leo. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa mBolea (TFRA) Dkt.Stephano Ngailo .Kiwanda hicho cha vijana watanzania kina uwezo wa kuzalisha tani 2,000 za mbolea kwa mwaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama mifuko ya mbolea ya asili ( Organic Fertilizer ) iliyozalishwa na kiwanda cha Guavay Dar es Salaam.Kulia ni Meneja Ubora wa kiwanda hicho Latifa Mafumbi. Mbolea hiyo ijulikanayo kama “HAKIKA” inatumika kwenye mazao ya parachichi,mpunga na vitunguu kwenye mikoa mingi nchini kwa sasa.

*******************************

( Picha na habari na Wizara ya Kilimo)

Wakati serikali ya Awamu ya Tano ikiendelea kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula wawekezaji wanahamasishwa kuanzisha viwanda vya mbolea ili nchi ijitosheleze .

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo (21.08.2020) ametoa wito huo kwa watanzania kuanzisha viwanda vya mbolea ambayo inahitajika kwa wingi zaidi wakati huu kilimo kikiwa ni biashara na kinaajili watanzania asilimia 58 na kuchangia malighafi za viwandani asilimia 65.

Kusaya ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kiwanda cha mbolea za asili na zilizoongezewa virutubishi ( Organic Fertilizer) cha Guavay kilichopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam ikiwa ni ziara yake ya kuhamashisha viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji wa mbolea.

Katibu Mkuu huyo amesema mahitaji ya mbolea hususan ya viwandani yameongezeka nchini kutokana na hamasa kubwa na wakulima kujitokeza kulima zaidi ikiwa ni mafanikio yaliyopatikana na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na sekta binafsi.

Kusaya ametaja takwimu za mahitaji ya mbolea kwa mwaka kuwa tani 664,000 wakati uzalishaji wa ndani kwenye viwanda umefika tani 30,000 ya mbolea hivyo kuwa na uhitaji mkubwa.

“ Nawahamasisha watanzania zaidi kujitokeza kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha mbolea ili wakulima wapate mbolea kwa gharama nafuu na karibu na wakulima “ alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo alisema hivi karibuni alifanya ziara mkoani Kagera na kupokea malalamiko ya wakulima kuuziwa mbolea aina ya UREA mfuko wa kilo hamsini kwa bei kati ya shilingi 80,000 na 90,000 hali inayowakwamisha kuongeza tija na uzalishaji.

Wakati huo huo ,Katibu Mkuu Kusaya amewashauri wakulima kote nchini kuwa na utaratibu wa kupata ushauri toka kwa Maafisa Ugani wa aina ya mbolea kwa mazao wanayolima kabla ya kwenda kununua ili wapate mbolea bora na yenye kuongeza tija ya uzalishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA) Dkt.Stephano Ngailo alisema uwepo wa malalamiko ya bei kubwa ya mbolea nchini unatokana na mbolea nyingi kuagizwa toka nje ya nchi.

Aliongeza kusema Tanzania kuna viwanda 12 pekee vinavyozalisha mbolea na kuwa uzalishaji huo ni chini ya 30,000 sawa na asilimia 6 ya mahitaji yote ya mbolea kwa mwaka hivyo kufanya bei kuwa kubwa kwa mkulima.

“ Kazi ya TFRA ni kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora na yenye gharama nafuu kwa wakulima ndio maana tunahamasisha wawekezaji kujitokeza kujenga viwanda vya mbolea kama ilivyo kwa kampuni ya Guavay” alisisitiza Dkt.Ngailo.

Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa kiwanda cha mbolea za asili na zilizoongezwa virutubishi cha Guavay cha Gongolamboto Dar es Salaam Meneja Ubora wa kiwanda hicho Latifa Mafumbi alimweleza Katibu Mkuu Kilimo kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea aina ya HAKIKA zinazorutubisha udongo.9

Latifa alisema uwezo wa kiwanda cha Guavay kwa sasa ni kuzalisha tani 2,000 za mbolea kwa mwaka na kuwa soko lao lipo kwenye mikoa ya Iringa,Njombe, Mbeya ,Arusha na Kilimanjaro.

“ Mbolea yetu ya HAKIKA inafanya vizuri zaidi kwenye mazao ya parachichi, mpunga na vitunguu kutokana na utafiti tuliofanya” alisema Latifa.

Alitaja changamoto ya mtaji kukuza uzalishaji wa mbolea ya asili umepelekea kampuni hiyo ya Guavay iliyoanzishwa mwaka 2014 na vijana wa kitanzania kushindwa kufikia mahitaji ya soko la mbolea ya Organic ya tani 20,000 kwa mwaka nchini.

Katibu Mkuu Kusaya ameanza ziara ya kukagua na kutembelea viwanda vya mbolea vilivyopo Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Manyara kukagua uzalishaji mbolea nchini

Post a Comment

Previous Post Next Post