Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Afya (MoU) ya miaka mitano itakayotekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, ikiwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.14 kupitia uwekezaji wa pamoja wa pande hizo mbili.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dar es Salaam Julai 1, 2026, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), amesema Marekani imekusudia kuwekeza takribani dola bilioni 1.34, huku Tanzania ikiahidi kuchangia zaidi ya dola bilioni 1.8 katika kipindi hicho.

Waziri Mchengerwa amesema makubaliano hayo yanaashiria hatua mpya ya ushirikiano unaojengwa katika misingi ya usawa, uwajibikaji na kujitegemea, badala ya utegemezi wa muda mrefu.

“Makubaliano haya si mwendelezo wa utegemezi bali ni ramani ya kutuondoa kwenye utegemezi. Ifikapo mwaka 2030 Tanzania ndiyo itakayobeba sehemu kubwa ya gharama za mfumo wake wa afya,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema Serikali itaendelea kugharamia mishahara ya watumishi wa afya, dawa, maabara na huduma nyingine muhimu kwa kutumia rasilimali zake za ndani, hatua inayotekeleza kwa vitendo falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere ya kujitegemea.

Aidha, Waziri huyo ameishukuru Serikali na wananchi wa Marekani kwa mchango mkubwa walioutoa kwa Tanzania kupitia programu mbalimbali za afya ikiwemo PEPFAR kwa zaidi ya miongo miwili.