Mwandishi Wetu,
Kamishna wa Magereza, C.P.A. J. Kavirondo, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na utekelezaji wa Mpango wa Mbolea za Ruzuku kwa wakulima nchini.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TFRA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), Kamishna Kavirondo amesema ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Magereza na TFRA umechangia kuimarisha shughuli za kilimo zinazofanywa na jeshi hilo kwa kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora na matumizi yake sahihi.
Aidha, ameiomba TFRA kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao, kuwajengea uwezo wafungwa kupitia kilimo na kuchangia katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, amemueleza Kamishna Kavirondo kuwa, TFRA inaendelea kusimamia ubora na upatikanaji wa mbolea nchini sambamba na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima na wadau wengine ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.


