Mwandishi Wetu,
Jamii ya Kabila la Wairaq wanaoishi mikoa ya Arusha na Manyara mwishoni mwa wiki iliyopita walifanya sherehe kubwa ikiwemo dua na sala maalum na kukemea laana iliyofanywa na wazee wao karne kadhaa zilizopita za kuwaua watoto wa kike waliopata ujauzito nje ya ndoa.
Tukio hilo kubwa lilifanyika jumamosi iliyopita katika makumbusho ya Urithi Geopark mjini Karatu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Daniel Sillo na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Sumaye.
Viongozi wa kutoka kabila hilo walipongeza jitihada kubwa zinazofanywa na watoto wa kike ambao kwa miaka sasa wamekuwa na maendeleo makubwa kiuchumi, kielimu na kisiasa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaendeleza wanawake ambao wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Naibu spika wa Bunge Mhe. Sillo aliwataka wananchi wa kabila hilo kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujiletea maendeleo sambamba na kulinda amani ya taifa.
Tukio hilo lilitanguliwa na ibada kubwa pamoja na mambo mengine kukemea laana iliyofanywa na Kabila hilo miaka kadhaa iliyopita ya kuua watoto wa kike waliopata ujauzito nje ya ndoa na kueleza kuwa laana ya kuwaua watoto wa kike waliopata ujauzito nje ya ndoa itaendelea kukemewa ili laana hiyo isiendelee kuumiza maisha ya kizazi cha sasa na kijacho cha kabila la Wairaqw.
Tukio hilo lililofanyika Makumbusho ya Urithi Geopark Karatu ni kuenzi historia na utamaduni wa makabila mbalimbali yanayounda Geopark ya Ngorongoro Lengai ambapo historia yao
imetunzwa katika makumbusho hiyo.
















