UNICEF YAIPA KONGOLE TANZANIA KWA KUPIGA HATUA KUBWA KWENYE HUDUMA YA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA

Mwandishi Wetu,

 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeipongeza Tanzania kwa kuendelea kupiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, hatua zinazotokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta hiyo na kuifanya nchi kuendelea kung’ara barani Afrika na duniani.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa UNICEF nchini, Bi. Elke Wisch, wakati wa mazungumzo na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Maji – Mtumba, jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalilenga kutathmini mafanikio ya ushirikiano uliopo na kujadili maeneo mapya ya ushirikiano yatakayochangia maendeleo zaidi ya sekta ya maji nchini.

Katika kikao hicho, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji na UNICEF zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya maji, usafi wa mazingira na afya (WASH) kwa lengo la kuboresha huduma za maji safi na salama pamoja na ustawi wa wananchi. Pande hizo pia zilijadili mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa programu na miradi ya WASH nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Aweso amesema UNICEF inaendelea kuwa miongoni mwa washirika wa maendeleo wanaoaminika na wa kimkakati katika Sekta ya Maji. Amesema kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji na miradi mingine, UNICEF imechangia takribani Dola za Marekani milioni 11.5 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kusaidia kuimarisha huduma za maji, usafi wa mazingira na afya ya jamii nchini.

Kwa upande wake, Bi. Elke Wisch ameipongeza Tanzania kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika sekta ya maji na usafi wa mazingira, akieleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali umeiwezesha nchi kuwa miongoni mwa mataifa yanayofanya vizuri katika eneo hilo barani Afrika na duniani. Aidha, ameahidi kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza mafanikio hayo kwa manufaa ya wananchi wote.

Katika kikao hicho, Waziri Aweso aliambatana na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, Naibu Katibu Mkuu, Bi. Rose Ambrose, pamoja na wakurugenzi na maafisa waandamizi wa Wizara ya Maji, huku ujumbe wa UNICEF ukiongozwa na Bi. Elke Wisch pamoja na wataalamu mbalimbali wa shirika hilo.


Post a Comment

Previous Post Next Post