Mwandishi Wetu,
Wizara ya Maji imepongezwa kwa jitihada za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Switbert Mkama (Mb) ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la Wizara ya Maji na Taasisi zake katika maonesho kuelekea siku ya mazingira katika viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
"Katika wizara zinazofanya vizuri basi na Wizara ya Maji imo, mmejitahidi sana kupeleka maji maeneo mengi nchini, sasa hivi kuna vijiji vipo mbali sana lakini vimefikiwa na huduma za maji safi, mmepunguza sana yale malalamiko ya wananchi kukosa maji, hongereni sana" Dkt. Mkama amesema.
Amewataka Bodi ya maji ya bonde la Wami-Ruvu kuhakikisha wanaendelea kulinda mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji ili visiharibiwe na shughuli za kibinadamu. Pia amewasisitiza kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowarahisishia wananchi wanaohitaji kuchimbiwa visima.
Maonesho kuelekea siku ya mazingira Duniani yameanza tarehe 1 Juni na yanatarajiwa kukamilika tarehe 5 Juni ikiwa ni Siku ya Mazingira Duniani.
Wizara ya Maji inashiriki maonesho pamoja na Taasisi zake ikiwamo DUWASA, DAWASA, RUWASA, Mfuko wa Taifa wa Maji na Bodi ya maji ya ya bonde la Wamiruvu.



