
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mazingira, Balozi Baraka Luvanda, wameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa mchango wake katika uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Viongozi hao walitoa pongezi hizo leo baada ya kutembelea banda la TFS katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayoendelea kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo walijionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo katika usimamizi wa rasilimali za misitu, uzalishaji wa miche ya miti, utalii wa ikolojia pamoja na ufugaji nyuki.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Muyungi alisema kazi inayofanywa na TFS ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za misitu zinatumika kwa njia endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunatambua mchango mkubwa unaotolewa na TFS katika uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa misitu yetu. Kazi hizi ni muhimu kwa ustawi wa mazingira, uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla. Tunawapongeza kwa juhudi zao na kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira,” alisema.
Alibainisha kuwa hatua za uhifadhi wa misitu na uhamasishaji wa upandaji miti zina mchango muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa na wananchi.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walipata maelezo kuhusu majukumu ya TFS katika kulinda misitu ya taifa, kuimarisha bioanuwai, kuendeleza utalii wa ikolojia na kusimamia shughuli za ufugaji nyuki ambazo zimeendelea kuwa chanzo cha kipato kwa jamii zinazozunguka maeneo ya misitu.
Kwa upande wake, Balozi Luvanda alisema ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na TFS katika kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na nyuki, akieleza kuwa shughuli hiyo ina manufaa makubwa kiuchumi na kimazingira.
Alisema ufugaji nyuki ni miongoni mwa shughuli zinazochangia uhifadhi wa misitu kwa kuwa unahitaji mazingira salama na endelevu, hivyo wananchi wanapaswa kuhamasishwa zaidi kushiriki ili kuongeza kipato huku wakichangia juhudi za uhifadhi wa mazingira.
“Bidhaa za nyuki zina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira, kipato, afya na lishe. Hii ni sekta inayostahili kupewa kipaumbele kwa kuwa inaunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi,” alisema.
Maonesho ya Wiki ya Mazingira yamekusanya taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazoshiriki kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya mazingira, huku banda la TFS likiendelea kuvutia wageni wengi wanaotaka kupata elimu kuhusu uhifadhi wa misitu, upandaji miti, utalii wa ikolojia na mazao ya nyuki.
