
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Australia zimedhamiria kuendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali yakiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira kwa ujumla.
Dhamira hiyo imeoneshwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Australia nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Jenny Da Rin.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma leo Juni 02, 2026, Mhe. Kwagilwa alimpongeza Mhe. Jenny kwa kujitoa kwake katika katika shughuli za hifadhi ya mazingira wakati akihudumu.
Alisema kuwa Tanzania inatambua uhusiano mzuri na nchi hiyo ya nchi hizo mbili hususan katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri dunia nzima.
Aidha, Mhe. Kwagilwa alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendeleza jitihada mbalimbali za kuhakikisha hifadhi ya mazingira inakuwa endelevu na kuwaletea fursa wananchi.
Alisema miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na za kuanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) huku akiomba ushirikiano katika kuwajengea uwezo watendaji kufikifikia malengo ya kuifikia jamii katika kuhamasisha kushiriki katika biashara ya kaboni.
Halikadhalika, alielezea namna Serikali inavyodhibiti taka kwa kuhamasisha jamii kutumia tena na kurejeleza hivyo kuwa na usimamizi mzuri wa taka, na kupitia hatua hiyo alitoa wito kwa nchi hiyo kushirikiana katika uwekezaji wa usimamizi wa taka.
Kwa upande wake, Balozi Jenny alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za elimu na mafunzo yanayotolewa na Serikali ya nchi hiyo ili kuchangia katika maendeleo ya Tanzania.
Aidha, Balozi Jenny alisema Serikali ya Australia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya kilimo, ikiwemo tafiti, usimamizi wa rasilimali maji, kuongeza uzalishaji wa mazao na utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo ya kilimo.
Pia, Balozi huyo alielezea dhamira yake ya kuendelea kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali wa Australia kuwekeza nchini Tanzania kwa manufaa ya mataifa hayo yote mawili.
