
KONDOA, DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Kondoa ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amesisitiza kuwa nyumba za ibada zinapaswa kuwa sehemu ya kuimarisha mshikamano, umoja na amani miongoni mwa wananchi na si kuwa chanzo cha migawanyiko katika jamii.
Dkt. Kijaji ametoa kauli hiyo Juni 04,2026 alipokuwa akifungua rasmi Msikiti wa Filimo uliopo Kata ya Mnenia, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kijaji amesema kuwa nyumba za ibada zina nafasi kubwa katika kujenga maadili mema, kuimarisha upendo na kukuza mshikamano wa kijamii, hivyo zinapaswa kutumika kwa malengo hayo kwa manufaa ya Taifa.
“Msikiti huu uwe chachu ya mshikamano ndani ya jamii yetu. Nawapongeza viongozi wa dini kwa kusimama katika haki na kuendelea kuhubiri amani na umoja miongoni mwa wananchi,” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, aliongeza kuwa kila mtu ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu katika jamii na mbele za Mungu, akibainisha kuwa maendeleo yanayopatikana katika Jimbo la Kondoa yanalenga kuwanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.
“Ninachokifanya ndani ya jimbo letu ni kwa ajili ya maendeleo ya Wakondoa wote. Tunapaswa kuendelea kushirikiana na kuishi kwa upendo ili kuleta maendeleo endelevu,” alisisitiza.
Vilevile , Dkt. Kijaji alitumia fursa hiyo kuwahamasisha waumini na wananchi wa eneo hilo kuendelea kujenga na kuendeleza nyumba za ibada ili zitumike katika kukuza maadili mema na kuimarisha imani katika jamii.
Katika hatua nyingine, amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vinavyohatarisha mustakabali wao, huku akiwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia amesisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto na vijana, akiwataka wazazi na walezi kuwajenga katika misingi ya maadili mema ili kuwa raia wema na wenye mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.
