Mwandishi Wetu,
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amewahakikishia wakulima nchini kuwa mbolea inapatikana kwa wingi na hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu upatikanaji wake katika msimu unaoendelea wa kilimo na msimu ujao.
Akizungumza leo tarehe 3 Juni, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maghala ya waagizaji wa mbolea jijini Dar es salaam , Mhe. Chongolo amesema lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha kuhusu hali ya upatikanaji wa mbolea nchini na kuwathibitishia wananchi kuwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo ni mzuri.
Amesema kampuni ya ETG Inputs Ltd pekee ina zaidi ya tani 47,000 za mbolea ambazo tayari zimesambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwemo Mbeya, Iringa na Kilimanjaro, huku gari zikiendelea kupelekwa katika mikoa mingine kulingana na mahitaji ya wakulima.
“Tumekuja kuwatembelea waagizaji wa mbolea nchini ili kujiridhisha kuhusu upatikanaji wa mbolea hata katika kipindi hiki ambacho shughuli za kilimo zimepungua katika maeneo mengi na kubaini kuwa mbolea ipo na itaendelea kupatikana kwa msimu huu na msimu ujao,” amesema Mhe. Chongolo.
Aidha, Mhe. Chongolo amesema serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea unaolenga kuhakikisha mkulima hapungukiwi pembejeo muhimu, huku timu maalum zikiendelea kufanya ufuatiliaji nchi nzima kujiridhisha kuwa mbolea inapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chongolo alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na udanganyifu au uchakachuaji wa pembejeo za kilimo, akisisitiza kuwa Serikali ipo macho na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kuhujumu sekta ya kilimo kwa kuuza pembejeo zisizokidhi viwango na zisizokuwa na ubora.






