
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Hussein Mohammed, amesema serikali inaendelea kuweka mkazo katika uwekezaji wa elimu yenye ubora, ujuzi na ubunifu ili kujenga vijana wenye uwezo wa kujiajiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza leo Aprili 10,2026 katika hafla ya kukabidhi cheti cha viwango vya kimataifa cha ISO 21001:2018 kwa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), amesema mafanikio hayo ni matokeo ya maono thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amewezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.
Amesema uwekezaji huo umeimarisha miundombinu na mifumo ya elimu katika kampasi mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza na Songwe, hali inayowezesha utoaji wa elimu inayozingatia mahitaji ya soko la ajira.
“Tunapaswa kuunganisha elimu na viwanda ili vijana wetu wawe sehemu ya uzalishaji na uchumi wa nchi. Hatuhitaji elimu ya vyeti pekee, bali elimu yenye ujuzi, ubunifu na tija,” amesema Hussein.
Aidha, amebainisha kuwa serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera zinazolenga kuongeza ufanisi wa elimu kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi na viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ashura Katunzi amesema kukabidhiwa kwa cheti hicho ni uthibitisho kuwa taasisi hiyo imefikia viwango vya kimataifa katika usimamizi wa elimu.
Ameeleza kuwa TBS itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu kuhakikisha zinazingatia ubora unaotambulika kimataifa, hali itakayosaidia kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo, David Masika, amesema kupata cheti hicho ni hatua muhimu katika safari ya kuboresha mifumo ya utoaji elimu na kuongeza ubora wa wahitimu.
Ameongeza kuwa taasisi itaendelea kusimamia utekelezaji wa mifumo hiyo kwa vitendo ili kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya maendeleo ya taifa.
Hafla hiyo imeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha elimu bora ya ufundi na teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.
