Na Mwandishi Wetu Dodoma ,
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta ya ualimu nchini kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP), kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maandalizi ya walimu ili kuhakikisha upatikanaji wa walimu bora watakaoinua ubora wa elimu mashuleni.
Akizungumza Aprili 9, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa “sekta ndogo ya ualimu ina nafasi ya kipekee kutokana na jukumu lake la kuandaa walimu wanaokwenda kufundisha watoto” amesistiza kuwa ubora wa maandalizi yao una mchango mkubwa katika ubora wa elimu inayotolewa nchini.
Prof. Nombo amebainisha kuwa Serikali imeweka mkazo katika kuwaimarisha wakufunzi na walimu watarajiwa ili kuzalisha walimu wenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya mfumo wa elimu wa sasa.
Ameongeza kuwa kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP),, vyuo vya ualimu vimenufaika na mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa vyuo na watumishi, pamoja na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa majengo mapya yanayozingatia uhimilivu wa mazingira. Akitaja Chuo cha Ualimu Kabanga kuwa miongoni mwa vyuo vinavyoongoza kwa kutumia nishati mbadala na kuzingatia uhifadhi wa mazingira, hatua inayotumika kama mfano katika miradi mingine ya elimu.
Aidha, Prof. Nombo amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia TESP yataendelea kudumishwa hata baada ya kukamilika kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo. Amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza takribani shilingi bilioni 140, huku wadau wa Global Affairs Canada wakichangia bilioni 92 katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora, Bi. Balbina Joseph, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP), umeleta maboresho makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira, usawa wa kijinsia, ujumuishi na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Ameongeza kuwa wakufunzi, watumishi na bodi za vyuo wamepata mafunzo yaliyoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kabanga, Bw. Phonce Mashibe, amesema chuo hicho kimenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia ujenzi upya wa miundombinu na uwekezaji katika mifumo ya nishati mbadala. Amefafanua kuwa matumizi ya biogas na nishati ya jua yamepunguza gharama za uendeshaji kwa kiasi kikubwa, zikishuka hadi asilimia 60.
Kwa upande wa wanafunzi, Marry Faustine Igulu, mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Bustani ngazi ya diploma, amesema kuwa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (Teachers Education Support Program – TESP),umeboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa maabara za sayansi, ukarabati wa mabweni, madarasa na maktaba. Ameongeza kuwa upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA umeongeza uwezo wa walimu tarajali kutumia teknolojia katika ufundishaji, hatua inayochangia kuinua ubora wa elimu nchini.

