TBS YASISITIZA VIWANGO KULINDA AFYA, USALAMA

 

 Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imesisitiza umuhimu wa matumizi ya viwango katika kuboresha ubora wa bidhaa na huduma, kuimarisha ushindani wa kibiashara na kulinda afya na usalama wa jamii.

Hayo yamejiri wakati wa sherehe za kitaifa za maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika yaliyokwenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa washindi wa shindano la uandishi wa insha la mwaka 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango TBS, David Ndibalema, amesema maadhimisho hayo yamewakutanisha wanafunzi na vijana kutoka vyuo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya viwango katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, alisema kupitia shindano hilo, vijana wanajengewa ubunifu, fikra chanya na ushiriki katika masuala ya viwango na ubora, ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Jaji Mkuu wa shindano hilo, Dr Jalia Muna, alisema tuzo hizo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika yanayoratibiwa katika ngazi ya bara na African Organisation for Standardisation (ARSO), yenye wanachama 44.

Akifafanua, alisema kuwa shindano hilo la kila mwaka lilianzishwa mwaka 2023 kufuatia uamuzi wa mkutano wa 49 wa ARSO uliofanyika Kenya, kwa lengo la kujenga uelewa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusu matumizi ya viwango katika biashara na maendeleo.

Kwa mujibu wa Dk Muna, TBS ilipokea jumla ya insha 522 kutoka kwa wanafunzi wa vyuo 33 vya elimu ya juu nchini, wakiwemo wanawake 230 na wanaume 292 na kwamba insha hizo zilichambuliwa na jopo la majaji sita kwa kuzingatia vigezo vya ARSO na hatimaye kupatikana washindi 10 wa kitaifa waliotangazwa na kupatiwa tuzo.

Mshindi wa kwanza alizawadiwa Sh 1.7 milioni, mshindi wa pili Sh1 milioni na mshindi wa tatu Sh 700,000, huku washindi wengine wote wakipokea Sh 300,000 kila mmoja.

Aliongeza kuwa insha tano bora zitawasilishwa ARSO kushindanishwa katika ngazi ya bara, ambapo insha bora zaidi itachapishwa katika tovuti rasmi ya shirika hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria, Candida Shirima, alisema siku hiyo pia ni fursa ya kuwakumbusha wazalishaji, watoa huduma na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika shughuli zao za kila siku.

Alisisitiza kuwa viwango ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa na huduma, pamoja na kuwezesha bidhaa za Tanzania kupenya katika masoko ya kikanda na kimataifa bila vikwazo.

Aidha, aliwahimiza wazalishaji kupata vyeti vya ubora kutoka TBS, akibainisha kuwa hatua hiyo huongeza uaminifu wa walaji, hupanua fursa za masoko na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.


Siku ya Viwango Afrika huadhimisha pia kuanzishwa kwa ARSO na kuonyesha mchango wa viwango katika kukuza biashara ya haki, maendeleo ya viwanda na uchumi endelevu barani Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post